Utata mkubwa umeibuka kuhusu waraka halisi wa
‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ uliosababisha Zitto
Kabwe kuvuliwa wadhifa wake wa Naibu Katibu
Mkuu wa Chadema na kikao cha Kamati Kuu ya
chama hicho kilichofanyika Novemba 20 - 22,
mwaka huu.
Baada ya juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa
Chadema, John Mnyika kuwaeleza wanahabari
kuwa waraka uliochapishwa katika magazeti na
mitandao ya kijamii, siyo halisi, aliyekuwa
Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha,
Samson Mwigamba amejitokeza na kuutetea huku
akidai kwamba huo unaodaiwa na uongozi kuwa
ndiyo halisi umeghushiwa.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
(Chadema), alivuliwa uongozi pamoja na
aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila
Mkumbo na Mwigamba kutokana na madai ya
kuandaa waraka huo ambao Chadema kimesema
ulikuwa unaeleza mbinu za uasi za viongozi hao
ambazo zingetumika wakati wa uchaguzi mkuu wa
ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume
na katiba, sheria na itifaki zake.
Katika tamko alilotoa jana, Mwigamba alidai
kwamba
kuna njama zinazofanywa na baadhi ya viongozi
wa Chadema ili kuubadili waraka halisi wa
‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ kwa lengo la
kupoteza maana yake, huku akisisitiza kuwa
waraka halisi hauna tatizo lolote.
Katika madai yake, Mnyika alisema waraka huo
unaosambazwa na kuchapishwa, si ule
uliowasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha
Kamati Kuu na kuahidi kuutoa waraka halisi ambao
una mambo makubwa na mengi zaidi.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo
huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa
katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na
mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu
mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,”
alisema.
Hata hivyo, jana Mwigamba alisema waraka halisi
ni ule ambao upo katika kompyuta mpakato
(Laptop) aliyonyang’anywa na wanachama wa
Chadema, Oktoba 25, mwaka huu, katika mkutano
mjini Arusha.
“Waraka uliosambazwa kwenye vyombo
mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni
sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma katika
magazeti ya jana (juzi), pamoja na nakala iliyopo
katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.”
Aliongeza: “Ili kuthibitisha kwamba waraka ule
ndiyo wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka
kwenye kompyuta yangu kwani waraka huo uliibwa
kutoka katika kompyuta hiyo ambayo nilirudishiwa
baada ya wao kuikagua na kukuta waraka huo
halisi.”
Mwigamba alisema waraka wake unatofautiana
kwa kiasi kikubwa na ule ambao Chadema
kinasema kuwa ndiyo halisi: “Lissu na wenzake
wana mpango wa kuuchakachua waraka huu, lakini
wamekwama.”
Alisema kuandaa waraka huo siyo uhaini kama
ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi wa
Chadema na kusisitiza kuwa ni waraka wa kusaka
ushindi katika uchaguzi halali ndani ya chama
hicho uliopangwa kufanyika Desemba mwaka huu
na baadaye kusogezwa hadi Juni mwakani.
“Wakati wa uchaguzi si ajabu kuwepo kwa
wanachama wanaounga mkono wagombea tofauti.
Nimekuwa karibu na Mwenyekiti wa Chadema,
Freeman Mbowe kwa miaka mingi, najua hata yeye
ana mikakati na wanaoshiriki mkakati wake ni
Lissu na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema,” alisema.
Alisema anashangazwa kwa kitendo cha Chadema
kuusambaza waraka huo, wakati ulikuwa ni
mpango wa siri kati yake, Dk Kitila pamoja na mtu
mwingine anayetajwa kwa jina la M2.
“Baada ya kugundua madhara ya kusambaza ovyo
waraka huo, sasa wameamua kuukana, waraka
wangu ni sahihi na unaeleza ukweli. Binafsi
nimefanya kazi ofisi ya makao makuu ya chama
kama Mhasibu Mkuu ningeweza kuanika mengi
lakini sijafanya hivyo kwa masilahi ya chama,”
alisema na kuongeza:
“Tunatambua kwamba viongozi wetu wanamchukia
Zitto na tangu siku nyingi walipanga kumfukuza.
Nawashauri watafute sababu nzuri za kumfukuza
uongozi na hata uanachama. Zitto hahusiki na
mkakati huu pamoja na kwamba alikuwa ndiye
mhusika mkuu, alikuwa hajui lolote.”
Jumamosi iliyopita, mama yake mzazi Zitto, Shida
Salum ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema alisema waraka huo ulikuwa
umeongezwa maneno.
“Hata ule waraka uliongezwa maneno baada ya
baadhi ya wanachama kumpora Mwigamba
`laptop’ yake alipokuwa mkoani Arusha katika
kikao cha Chadema,” alisema bila kutaka
kufafanua ulibadilishwa vipi, licha ya kuwataja kwa
majina waliohusika kuubadili wakiwamo wabunge
wawili wa chama hicho na viongozi wa ngazi za
juu.
Sitoki Chadema
Kuhusu hatima yake ndani ya Chadema,
Mwigamba alisema hana mpango wa kuondoka
hata baada ya kuvuliwa uongozi, huku akisisitiza
kuwa hakusudii kuomba radhi kutokana na
kuandaa waraka huo.
Alisema hakusudii kuhama kwa kuwa ana historia
ndefu na Chadema na anaamini kuwa ndicho
mkombozi wa Watanzania.
“Nimekuwa kiongozi wa kata, wilaya, mkoa hadi
taifa. Nimetumia muda wangu mwingi na hata
kuhatarisha maisha yangu kwa ajili ya chama hiki,
siwezi kuondoka kutokana na tofauti za
kimitazamo na viongozi wangu,” alisema.
Mwigamba, ambaye alikuwa mfanyakazi katika
Mahakama ya Kimataifa inayosikiliza Kesi za
Mauaji ya Halaiki ya Rwanda (ICTR) na baadaye
kujiondoa ili ajikite kwenye siasa, alisema ana
imani yanayotokea sasa katika chama hicho
yatapita salama.
Mwananchi
Thursday, 28 November 2013
WARAKA HALISI WA MKAKATI WA MADILIKO 2013 CHADEMA UTATA MTUPU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment