KATIKA moja ya mambo yaliyojitokeza katika mgogoro wa
uongozi wa Chadema, ni tathmini ya nguvu za aliyekuwa
Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto dhidi ya kinachoitwa
udhaifu wa Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Freeman
Mbowe na uongozi wake.
Tathmini hiyo ambayo aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo jana ameiita kuwa ni siri
iliyowekwa wazi kwa makosa ya kijinga, imeeleza namna
kiongozi huyo alivyoandaa mkakati wa kumuondoa Mbowe
madarakani kidemokrasia, kupitia nguvu za Zitto.
“Nani tumuunge mkono kuchukua nafasi ya Mkuu
(Mbowe).Utangulizi huo (udhaifu wa Mbowe) unaoonesha
kinagaubaga kwamba tunahitaji mabadiliko na hatua
iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta
mabadiliko tunayohitaji. “Ni vema ikazingatiwa kwamba
mtu ambaye tungemuunga mkono lazima awe mwenye
uwezo mkubwa kuliko tunayetaka kumtoa (Mbowe).
Awe ana sifa za kiuongozi na zaidi sana awe na uwezo wa
kupambana na mkuu aliyeko. “Katika kuchunguza ndani ya
taasisi (Chadema), tuliridhika kwamba Mtendaji Mkuu
Msaidizi (Naibu Katibu Mkuu, Zitto), ana sifa zote
tulizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana udhaifu
wake.
“Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa Mtendaji Mkuu Msaidizi
unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo,” umeeleza mkakati
ambao Dk Mkumbo amekiri kuuandaa na kusisitiza hajutii
kazi hiyo aliyoiita ni ya matamanio ya mabadiliko ndani ya
Chadema.
“Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo kwamba
matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na
kuandaa mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za
kidemokrasia ni uhaini,” alisisitiza Dk Mkumbo alipokutana
na waandishi wa habari Dar es Salaam kukiri kupanga
kumuondoa Mbowe na uongozi wake madarakani.
Udhaifu wa Mkuu Mbowe anadaiwa na Dk Mkumbo kwa
kuondoa kipengele cha Katiba ya chama kinachomzuia
kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya
vipindi viwili vya miaka mitano mitano, ili aongoze kwa
zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
“Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini
kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika
jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na
wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye
athari zisizomithilika kwa taasisi yetu,” alisema Dk
Mkumbo ambaye alimuomba msamaha Mbowe kwa
kumweka wazi namna hiyo.
Katika uchaguzi mdogo, Kitila anasema matokeo ya
Chadema yamekuwa dhaifu na kwamba hiyo ni ishara
kwamba mabadiliko yanahitajika.
Alisema kuwa tangu uongozi wa Mbowe uingie madarakani,
kumefanyika chaguzi ndogo mara nane na uchaguzi wa
wawakilishi kwenye Baraza la Wawakilishi lakini katika
uchaguzi huo, Chadema imeshinda mara mbili tu, sawa na
asilimia 25.
“Kwa kifupi ushindi ambao tumekuwa tukiupata katika
chaguzi ndogo, haulingani na ukubwa wa hamasa kwa
taasisi yetu ulivyo mitaani. Hii ni kwa sababu tumekuwa
tukitumia mbinu hizo hizo katika kila uchaguzi. Aidha, tu
wepesi mno wa kuridhika na kujisifu kwa mafanikio
madogo badala ya kukaa chini na kutafakari kwa kina
mahala tunapojikwaa,” anasema Dk Mkumbo katika
mkakati wake wa kumng’oa Mbowe.
Ubadhirifu wa fedha Dk Mkumbo anasema hakuna mtu
anayejua fedha zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu
watatu; yaani mkuu kabisa Mbowe, Mtendaji Mkuu, Dk
Willibrod Slaa na Mkuu wa Fedha kwenye taasisi hiyo.
“Kuna hata michango ya watu binafsi kama yule Mtanzania
mwenye asili ya Kihindi, (Mustafa Sabodo) hizo nazo
hazijulikani zimechukuliwa lini kwa mfumo gani,
zikatunzwa wapi na hatimaye zimetumikaje.
“Kwa kiasi kikubwa mkuu aliyepo anatengeneza mazingira
yaleyale ya mwaka 2005 na 2010 ya kutaka chama kiwe
hakina fedha ili ikifika wakati wa uchaguzi kimpigie
magoti.
Kisha atatoa fedha bila kumbukumbu zozote na mara
baada ya uchaguzi atapeleka lundo la madeni na kudai
alipwe fedha aliyokikopesha chama wakati wa uchaguzi,”
alidai Dk Mkumbo.
Akifafanua Dk Mkumbo alidai baada ya uchaguzi mkuu wa
taasisi (Chadema), baadhi wa wapambe wa mkuu walileta
deni kubwa la takribani Sh milioni mia tano wakidai kuwa
walikikopesha chama. “Taasisi imewalipa fedha zote hizi
kwa muda wa mwaka mmoja. Sasa anatengeneza
mazingira hayo hayo kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka
2015,” anasema Dk Mkumbo.
Dk Mkumbo anaendelea kuweka wazi kuwa mkuu wa
taasisi bila aibu, amekuwa mnunuzi wa vifaa vyote vya
chama nje ya nchi kwa bei anayoijua mwenyewe na
ambayo haihojiwi popote.
“Huu ni mfano wa wazi wa mgongano wa kimaslahi jambo
ambalo ni hatari kwa kiongozi mkubwa wa taasisi kama
yetu, inayojitambulisha katika kupinga vitendo vya ufisadi
na uvunjifu wa maadili ya uongozi kwa ujumla,” alisema.
Kumpata Zitto “Baada ya utangulizi huo unaoonyesha
kinagaubaga kwamba tunahitaji mabadiliko, hatua
iliyofuata ilikuwa ni kuangalia nani anaweza kuleta
mabadiliko tunayohitaji. Ni vema ikazingatiwa kwamba
mtu ambaye tungemuunga mkono lazima awe ni mtu
mwenye uwezo mkubwa kuliko tunayetaka kumtoa,”
ameeleza Dk Mkumbo.
Amedai mtu waliyepanga kumweka madarakani ni mwenye
uwezo wa kiuongozi na zaidi awe na uwezo wa kupambana
na mkuu aliyeko. “Tukileta mtu asiyefahamika sana
kwenye mifumo ya taasisi yetu hata kama angekuwa mzuri
kiasi gani, hatachagulika na mkuu aliyeko atarudi kwa
urahisi na kuendelea kuididimiza taasisi,” ameonya Dk
Mkumbo katika mkakati huo.
Katika kuchunguza ndani ya taasisi, Dk Mkumbo anadai
waliridhika kwamba Mtendaji Mkuu Msaidizi ana sifa zote
walizozitaja hapo juu ingawa kila mwanadamu ana udhaifu
wake.
“Ni dhahiri pia kwamba udhaifu wa mtendaji mkuu msaidizi
unarekebika kuliko wa mkuu aliyepo.“ Sifa za Zitto “Ni
kiongozi anayeweza kuongoza taasisi bila kujenga
makundi akijali zaidi kazi ya taasisi kuliko maslahi binafsi.
Ameonesha kwa vitendo kwamba hana maslahi binafsi kwa
kuwa tumeshuhudia akifanya kazi nyingi za taasisi bila
kudai malipo kwa njia ya posho ama vinginevyo,” anaeleza
Dk Mkumbo.
Amedai kuwa kiongozi huyo anaheshimika na viongozi wa
ndani na nje ya taasisi, jambo ambalo ni la muhimu sana
kwa ustawi wa taasisi na kwa yeye kuwa mkuu wa taasisi,
wanatarajia wakubwa wengi sana kutoka nje ya taasisi
wataamini na hata kujiunga katika kuhakikisha lengo la
taasisi linafanikiwa.
“Ni msomi wa kiwango cha juu na mwenye uwezo mkubwa
katika kuchanganua mambo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii
na kimichezo, jambo ambalo ni muhimu kwa kuwa ni hatari
kuwa na kiongozi asiye na ujuzi wa kutosha kwenye
masuala kama hayo. Ndani ya taasisi anakubalika kwa
makundi yote ya vijana, wazee na akina mama,” alieleza
Dk Mkumbo.
Amedai uelewa wa kiongozi wanayemtaka wa mambo ya
kiuchumi ni muhimu kwa taasisi kwa sasa kwa kuwa
taasisi inahitaji kuja na vyanzo vipya vya mapato ikiwa
inahitaji kufanikiwa. “Mkuu aliyepo si kwamba ameishiwa
bali hana mbinu za maana za kuiimarisha taasisi kimapato
kwa ajili ya malengo yake ya mbele.”
---Habari Leo.
Monday, 25 November 2013
Nguvu za Zitto, udhaifu wa Mbowe ndani ya Chadema...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment