SHABANI MATUTU NA PATRICIA KIMELEMETA
UMOJA
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umedai kunasa waraka wa Ofisi ya Rais
Ikulu unaoonyesha Serikali imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kampeni
ya kuwezesha Katiba inayopendekezwa ipitishwe kwa kupigiwa kura ya
ndiyo katika kura ya maoni.
Katibu
Mkuu wa Ukawa ambaye pia ni Katibu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa,
alidai Dar es Salaam jana kuwa kampeni hiyo itafanywa kupitia vyombo
vya habari kuwahamasisha wananchi waweze kupiga kura ya ndiyo na
kuipitisha kwa urahisi Katiba inayopendekezwa.
Waraka
huo alidai kwamba unatoka Ikulu kwenda kwa Wizara ya Habari Utamaduni
na Michezo na kuelekeza kazi hiyo inatakiwa kuanza wiki hii zikipatikana
Sh milioni 50 za kuanzia.
“Ofisi ya Rais Ikulu imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kuhamasisha wananchi waweze kuipigia kura ya ndiyo Katiba pendekezwa.
“Lengo ni kutaka kuipitisha Katiba hiyo bila ya kuwaelimisha wananchi jambo ambalo ni kinyume na sheria,” alisema Dk. Slaa.
Alisema
suala hilo ni kinyume na sheria kwa sababu wanaohusika na utangazaji
au uhamasishaji wa Katiba mpya ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
siyo Ofisi ya Rais Ikulu.
Alidai ofisi hiyo imeandaa Kamati ya Kudumu ya Habari ya kusimamia mpango wa kuelimisha umma hadi muda wa kura ya maoni.
VYOMBO VYA HABARI
Dk.
Slaa alidai baadhi ya vyombo vya habari vimetengwa kwa ajili ya kazi
hiyo zikiwamo redio, magazeti, mitandao ya jamii na televisheni
mbalimbali kuhakikisha mpango huo unafanikiwa.
Alidai
wahariri wa vyombo hivyo wametengewa fedha kuhakikisha wanatumia vyombo
vyao kutenga vipindi vya kutoa elimu kwa wananchi juu ya suala hilo.
Dk.
Slaa alidai vipindi hivyo vitaongozwa na baadhi ya watu walioandaliwa
kufanya kazi hiyo wakiwamo wasomi kutoka vyuo vikuu nchini; baadhi yao
ni wale waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
WASOMI
Dk.
Slaa alidai wasomi hao watalipwa Sh 500,000 kwa kila kipindi
watakachoshiriki katika muda wa wiki 22 kuhakikisha suala hilo
linafanikiwa.
“Wameamua
kuwachukua baadhi ya wasomi kutoka vyuo vikuu, tena baadhi yao walikuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuendesha vipindi hivyo kwenye
media mbalimbali nchini,” alisema.
NGOMA, VIKUNDI VYA UTAMADUNI
Dk.
Slaa alidai katika kampeni hiyo pia zitatumiwa ngoma na vikundi vya
utamaduni vya asili wakiwamo maofisa utamaduni wa maeneo mbalimbalia
kwa ajili ya kuvikusanya pamoja vikundi hivyo.
Njia
nyingine alizitaja kuwa ni kubandika mabango katika miji mikuu ya mikoa
kuongeza uelewa wa Katiba inayopendekezwa ili wananchi waipigie kura ya
ndiyo.
Alipotafutwa
kwa simu kuzungumzia madai hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ofisi ya
Rais Ikulu, Salva Rweyemamu alisema; “nitakupigia baadaye”.
Hata hivyo hakuweza kupiga na alipotafutwa mara kadhaa baadaye simu yake haikupatikana hadi tunakwenda mtamboni.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment