Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging
DUNIA hii basi tena! Ni
tukio la kusisimua ukilisoma mwanzo hadi mwisho lakini ni la kikatili
sana! Ni lile la ndugu wawili warembo, dada na mdogo wake kukutwa
wamekufa kwa kunyongwa ndani ya nyumba aliyokuwa amepanga mmoja wao huku
muuaji akidaiwa alivaa taulo lenye weupe wa kufifia akitokomea zake.
Nuru Tumwaga enzi za uhai wake.
ENEO LA TUKIO
Tukio
hilo la kusikitisha lilitokea hivi karibuni kwenye Mtaa wa Mji Mpya,
Kata ya Azimio wilayani Temeke jijini Dar es Salaam ambapo warembo hao,
Mariam Buruhani (39) na dada yake Nuru Tumwaga (42) (pichani) walikutwa
wamekufa katika nyumba hiyo aliyopanga Mariam.
UWAZI LAFUATILIA
Uwazi
kama lilivyo kawaida yake, baada ya kuipata taarifa za kuwepo kwa vifo
hivyo vya usiku mmoja, lilianza kufuatilia hatua kwa hatua.Kwa mujibu wa
ndugu mmoja, mchana wa kuelekea siku ya tukio ambayo ni Jumamosi usiku,
marehemu wote walionekana wakiwa wazima wa afya ambapo Mariam alikuwa
kwenye saluni yake ya kike na Nuru akiendelea na shughuli zake za
kuwaremba wanawake wenzake.
Ikadaiwa
kuwa, nje ya saluni ya Mariam kulikuwa na gari dogo jeusi ambalo huwa
linapaki maeneo hayo kila wakati ikisemekana mmiliki wake ni bwana wa
Mariam ambaye jina halikufahamika mara moja.
Mariam Buruhani enzi za uhai wake.
GARI LAONDOKA
Ndugu huyo aliongeza: “Baadaye lile gari liliondoka na kwenda kusikojulikana, Mariam alibaki saluni.
MARIAM AFUNGA SALUNI
“Ilipofika
saa moja usiku, Mariam alifunga ofisi na kwenda nyumbani kwake akiwa
ameongozana na Nuru ambaye alikuja jijini Dar kwa Mariam akitokea
Mtwara. Mariam ni mtoto wa mama mkubwa wa Nuru.“Baada ya kufika
nyumbani, Mariam alitoka kwenda dukani kwa ajili ya kununua mahitaji
ambapo alinunua juisi chupa tatu, mafuta ya taa na mahitaji mengine.”
INAVYODAIWA
Habari
zaidi kutoka kwa ndugu huyo zilidai kuwa, wiki moja nyuma marehemu
Mariam aliomba hati ya nyumba yake iliyoko Tandika kwa lengo la kuiuza
kwa vile alipata mteja.
“Siku
ya tukio, ilikuwa mteja wake afike kwa ajili ya ununuzi wa nyumba hiyo
lakini kwa bahati mbaya hakufika, alikuwa na matatizo.
Wanafamilia wakiwa na nyuso za simanzi.
“Kesho
yake, Jumapili saa sita mchana yule mteja alifika nyumbani kwa kaka wa
marehemu aitwaye Abdallah ambapo ni jirani na alipopanga Mariam, kaka
akamtuma mtoto wake kwenda kumwita shangazi yake (Mariam).“Lakini cha
kushangaza, mtoto huyo alichelewa kurudi ndipo kaka mtu na watu wale
waliamua kufuatilia,” alisema ndugu huyo.
MSIKIE KAKA MTU
“Tulipoona
mtoto harudi tukafuata, kufika tulishtuka sana kumkuta Mariam amelala
sebuleni amekufa, kuingia chumbani tukamkuta Nuru naye amelala kitandani
amekufa,” alisema kaka mtu.
MAUZO YA NYUMBA YANATAJWA
Kaka wa Mariam aliendelea kusema: “Tunaamini muuaji alijua marehemu ameuza nyumba na pesa anazo ndani.”
VYANZO ENEO LA TUKIO.
Naye
jirani na Mariam (aliomba jina lake lihifadhiwe) akizungumza na Uwazi
kuhusu mazingira ya kunyongwa kwa warembo hao alisema:
Waombolezaji wakiwa msibani.
“Usiku
wa tukio mimi nilichungulia dirishani baada ya kusikia mtu akitembea,
nikamuona mwanaume amevaa taulo lenye weupe wa kufifia. Nilipomwangalia
vizuri nikagundua ni bwana’ake da’ Mariam maana namfahamu.
“Baada
ya muda nikasikia mngurumo wa gari, nikachungulia tena nje nikaliona
gari ambalo ni la bwana’ke da’ Mariam likiondoka eneo hilo.“Sikujali,
niliamini tuko salama. Nilipoamka asubuhi nikawa namuona mtu amelala
sebuleni kwa Mariam, nikajua kwa vile ni Jumapili, huenda amepumzika,
sikujua ni marehemu Mariam mpaka kaka yake alipofika na watu wenegine na
kubainisha kuwa, kumbe wote waliolala ndani humo walikuwa wameuawa,
inauma sana.”
SERIKALI YA MTAA
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Azimio, Wadudi Mlangwa
akizungumza na waandishi wetu ofisini kwake alisema yeye ni kati ya
viongozi wa mwanzo kufika eneo la tukio baada ya kupigiwa simu na kaka
wa marehemu.
Mwili wa Nuru ukiswaliwa kwa ajili ya mazishi.
“Tulipofika
tulikuta mwili wa Mariam uko sebuleni na mwili wa Nuru uko chumbani,
wote wakiwa wameaga dunia. Hapo ilikuwa saa saba na nusu mchana wa
Jumapili Oktoba 26, mwaka huu,” alisema.Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa,
baada ya kuthibitisha hali hiyo aliagiza miili hiyo isiguswe hadi
polisi wafike kwa hatua zaidi.
UCHUNGUZI WA AWALI WA KIDAKTARI
Uchunguzi
wa awali uliofanywa na madaktari wa Hospitali ya Temeke jijini Dar
ulibaini kuwa, marahemu hao walinyongwa kwani shingo zao zilikutwa
zimepindia upande.
NINI KILIFANYIKA BAADA YA MAUAJI?
Uchunguzi
wa gazeti hili ulibaini kuwa baada ya mauaji hayo, chumba cha marehemu
Mariam kilionekana kupekuliwa kila sehemu. Baada ya upekuzi huo,
mpekuaji alichukua redio, tivii na vitu vingine ambavyo vinaendelea
kufuatiliwa na polisi.
Mwili wa Mariam Buruhani ukiswaliwa kwa ajili ya mazishi.
MAZISHI YAO
Mariam
alizikwa Jumatatu ya Oktoba 27, mwaka huu kwenye Makaburi ya Wailesi
Temeke, Nuru alisafirishwa siku hiyohiyo na kwenda kuzikwa kwao, Mtwara
Jumanne ya Oktoba 28, 2014.
KAMANDA WA POLISI
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, SACP Kihenya wa Kihenya
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, “Tunamtafuta mtu aliyehusika na
mauaji hayo ambaye anatajwa alivaa taulo,” alisema.
No comments:
Post a Comment