MFANYAKAZI
wa kujitolea ambaye alitumia Paundi 5,000 (sawa na Sh 12,500,000 za
Tanzania) kumleta mkewe mpya kutoka Jamaica hadi Uingereza amejikuta
akiumizwa moyo baada ya mke huyo kumuacha dakika 20 tu baada ya kufika
nyumbani kwa mumewe.
Johnny
Gannon alitumia maelfu ya fedha kumtafutia Visa Patrice Chambers (24)
ili waweze kuishi kama mke na mume katika nyumba yake iliyopo Perth,
Scotland, lakini mara tu baada ya Patrice kuwasili Perth, alimtuma
Gannon (57), kwenda kununua chakula.
Hata
hivyo aliporudi msichana huyo alinyakua mabegi yake na kumwambia
anaondoka. Dakika 20 baada ya kuwasili nyumbani kwao, msichana huyo
alikimbilia kwenye gari na kisha kupanda treni na kutokomea.
Mumewe amegundua pia Patrice amemwachia bili ya paundi 500 ( sawa ni Sh 1, 250,000)katika simu yake ya mkononi.
Gannon
aliyeumizwa moyo, alifunga ndoa na Patrice mjini Jamaica mapema mwaka
huu, akiamini mkewe mpya amekimbilia Bristol kukutana na mpenzi wake
ambaye ni Mjamaica ambaye walichonga mpango wa kutoroshana.
Alilieleza
gazeti la Daily Mirror, “ nilikuwa na matarajio makubwa ya kuishi
maisha yangu yote na Patrice , lakini nadhani alikuwa ameshaweka mipango
yake ya kufanya hili… uhusiano wangu na yeye sio wa kuonana kwenye
baruapepe. Nimemfahamu kwa miaka miwili na alionekana kuwa mkweli
kwangu. Amenitumia na najisikia kudhalilishwa.
Nilikuwa
na maono ya furaha mbele yetu. Najiona mjinga.” Gannon alikuwa akienda
mara kwa mara Jamaica kwa ajili ya mapumziko na ndipo alipokutana na
Patrice miaka mitatu iliyopita. Rafiki aliwakutanisha, pamoja na
utofauti wa miaka 33 alimpenda mara baada ya kukutana kwa mara ya kwanza
katika baa ya hoteli iliyopo Treasure Beach.
“Alikuwa
akiendesha baa ndogo na nilikuwa nikikaa naye pale. Ni msichana mwerevu
na mimi nilifikiri ni patna anayestahili katika maisha yangu.”
“Ni
kweli nilikuwa nikijifinya mara nyingine maana nilikuwa siamini jinsi
nilivyokuwa na bahati kupata mwanamke kijana mzuri. Lakini uhusiano wetu
ulikuwa ukiendelea vizuri kila muda ulivyokuwa ukienda vizuri, kwa hiyo
sikutegemea kuumizwa kwa kiasi hiki,” alisema.
Alisikia
kutoka kwa rafiki wa Patrice kuwa binti huyo alikuwa na rafiki wa kiume
Uingereza lakini alipomuuliza alijitetea kuwa alikuwa ni jamaa wake wa
zamani.
Mapenzi
aliyokuwa nayo kwa msichana huyo yalimfanya amuamini na aliendelea
kuonana naye kila alipokuwa akienda Jamaica. Gannon anasema Patrice ndio
alianza kugusia habari za kufunga ndoa na sherehe iliandaliwa katika
safari yake moja alipokwenda Jamaica.
Alilipia
gauni la bibi harusi na hela ya kutengenezea nywele kwa ajili ya siku
ya harusi na aliporudi Scotland alianza kushughulikia viza kwa ajili ya
msichana huyo. Mwisho Gannon alimtumia Patrice paundi 700(1,750,000) kwa
ajili ya kushughulikia makaratasi nchini Jamaica na alimtumia fedha
zaidi baada ya kudai kaibiwa. Mwaka huu pekee Gannon ametumia zaidi ya
Paundi 4,000 (sawa na Sh 10,000,000 za Tanzania) kwa ajili ya Patrice.
Marafiki
waliwapokea Gannon na mkewe walipowasili kwa ndege katika uwanja wa
Edinburgh kwa ajili ya kwenda kuanza maisha yao mapya kama mke na mume
lakini Patrice alimwambia hataki kuishi naye na Gannon aliporudi kutoka
kufanya manunuzi kwa ajili ya mkewe alimpeleka kwenye stesheni ya treni.
Gannon
ametoa taarifa Polisi na amepanga kuwasiliana na Wakala wa Uhamiaji
Uingereza na anafikiria atamwambiaje mama yake kuhusiana na fedheha
hiyo.

No comments:
Post a Comment