Tuesday, 23 September 2014

ASKOFU WA KATOLIKI AELEZA NJIA MPYA KUZUIA KATIBA







Makamu wa Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi.






MAKAMU wa
Rais Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Severin Niwemugizi,
amesema maoni yaliyotolewa na Jukwaa la Wakristo Tanzania (TCF) juu ya
Bunge Maalumu la Katiba, hayajatekelezwa na hivyo watapita kwa
Watanzania na waumini wao kuwaeleza nini cha kufanya.
Jukwaa hilo lilikutana Agosti 27 hadi
28, mwaka huu na kujadili hatima ya Bunge hilo na kutoa mapendekezo
sita, moja ikiwa ni kusitishwa kwake.
Akizungumza na paparazi jana,
Niwemugizi  ambaye pia ni mjumbe wa TCF, alisema: “Tunaona Bunge bado
linaendelea na Serikali iliyopo madarakani inaendelea na mipango yake,
haiheshimu wala haitekelezi ushauri unaotolewa.
“Sauti nyingi haziridhiki na yale
yanayotendwa na Bunge Maalumu la Katiba, hawajui ni kiasi gani
Watanzania wameshapevuka na wanatambua haki zao.”
Alisema wamejipanga kurudi kwa
Watanzania kuwafahamisha na kuwafundisha ili watambue haki na wajibu wao
hali itakayowasaidia kujua njia sahihi ya kufanya.
“Wanaweza kutudharau kwamba sisi hatuna
chochote, kwakuwa hawajali tuliyopendekeza, tutarudi kwa watu wetu
tunaowaongoza, kitakachotokea hatujui.
“Sisi tunaamini kurudi kwa Watanzania ni
sehemu pia ya injili kwa sababu kuna injili ya jamii, na tutawafundisha
watambue haki na wajibu wao na namna sahihi ya kufanya,” alisema.
Askofu huyo alisema wanachotaka
Watanzania ni kuona mambo yakienda vizuri, hivyo kama viongozi wanakataa
ushauri unaotolewa, Watanzania wataamua cha kufanya.
Kuhusu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la
Katiba, Samuel Sitta, askofu huyo alisema amejidhalilisha kwa kauli zake
za kejeli ndani ya Bunge hilo.
“Mkishakuwa na viongozi wenye dharau na
kejeli, hapo nchi imekwisha kabisa. Sitta amejidhalilisha kwa kauli
zake, hasa ukizingatia kuwa na yeye anatajwa kutaka kugombea urais, sifa
zake zinazidi kupungua,” alisema.
Jukwaa hilo linaundwa na Baraza la
Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste (CPCT),
Jumuiya ya Kikristo (CCT) na Makanisa ya Kisabato (SDA).
Tamko la jukwaa hilo lililotolewa Agosti
28, mwaka huu, lilisema mjadala wa Bunge hilo umeondoa maoni
yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya
Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wao.
“Wamewezesha maoni na maslahi ya chama
tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu
na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia
ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa
wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora,” inasema sehemu ya tamko
hilo.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa hilo lilitoa mapendekezo sita likitaka yafanyiwe kazi.
MAPENDEKEZO YA JUKWAA
1. Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria)
irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote
kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na
kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.
2. Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea
lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio
kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.
3. Mchakato wa Katiba usimamishwe ili
kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano mwafaka, Uchaguzi Mkuu na
wa Serikali za Mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977
yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka
kifungu kitakacholinda rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye
kuendelea na mchakato wa Katiba.
4. Baada ya Bunge Maalumu la Katiba
kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa
mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia
ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge
la Katiba.
5. Wananchi waendelee kusoma na kujadili
maoni yaliyoko katika rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia
kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga
kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo
kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.
6. Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe
na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza
na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla
hadi Katiba mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.
Tamko lilisema: “Jukwaa la Wakristo
Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba
Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako, hasa
katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba mpya.
“Tunakuomba uahirishe mchakato
unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha
sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya
mshikamano, umoja na amani ya taifa letu.
“Ifahamike kuwa Wananchi wa Tanzania
wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba
uepushe wananchi wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi
kwa kuwa tu chama hicho kimeyapuuza na kimekataa maoni yao waliyotoa
kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa
nchi.
“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa.
“Wamejawa na udhalimu wa kila namna,
uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,
wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari,
wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na
ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;
si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao. (Rejea Warumi 1: 28-32)
“Ikumbukwe kuwa Rasimu ya Pili ya Katiba
ni waraka halali na rasmi na ndiyo mawazo ya Watanzania na tunahimiza
kuwa Katiba ni ya wananchi na inahitaji maridhiano na siyo ubabe.”


No comments:

Post a Comment