MWANAMUZIKI wa nyimbo za Injili nchini, Rose Muhando anasakwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar baada ya mchungaji mmoja wa Kinigeria anayefanya shughuli zake nchini DR Congo, Kabagambe Tchanda kumshitaki akidai kumlipa fedha ili akafanye onesho badala yake akaingia mitini.
Uchunguzi uliofanywa na paparazi ndani
ya jeshi hilo, umegundua kuwa kuna madai hayo na kwamba mchungaji huyo
alitua jijini Dar na kufanya mazungumzo na Rose kwa ajili ya kwenda
kutumbuiza nchini DR Congo, Julai mwaka huu katika mkutano uliohusisha
wageni kutoka Ulaya na kukubaliana amlipe Dola za Marekani 5,000 (zaidi
ya shilingi milioni 8).
Kwa mujibu wa chanzo, ilidaiwa kuwa
mchungaji huyo alimkabidhi Rose dola 1,900 kama utangulizi na kubaki
dola 3,100 ambazo angemlipa baada ya onesho. Makabidhiano hayo
yalifanyika Magomeni ya Mwembechai jijini Dar.
Kutokana na sekeseke hilo, paparazi
alimsaka mchungaji huyo na alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa madai hayo,
alikiri na kusema alimuamini sana Rose lakini cha ajabu mambo yamekuwa
tofauti kwa kuwa hakufika kwenye tamasha.
Mchungaji huyo aliendelea kudai kuwa,
kinachomuuma zaidi ni kwamba, Rose hataki kumrudishia fedha zake na
badala yake amekuwa akimzungusha na chenga kibao.
“Siamini kabisa kama Rose angeweza
kufanya vile maana yeye ni mtumishi wa Mungu, sasa kwa nini afanye mambo
yasiyompendeza Bwana? Nashangaa sana, sijui hata ni nini kimemuharibu
huyu! Nikimpigia simu akipokea kesho haziishi.
“Anashindwa kuwa na utu maana mimi
nimeishiwa fedha naishi kwa shida hapa nchini, angenipatia hizo pesa
zingenisaidia sana maana ujio wangu huu ni kwa sababu ya kudai hizo pesa
tu, ndiyo maana nikaamua kulifikisha suala hili kwenye vyombo vya dola
baada ya kuona hatuelewani,” alisema.
Ili kuweka sawa mzani wa habari,
paparazi alimtafuta Rose Muhando kupitia simu yake ya mkononi ambayo
iliita bila ya kupokelewa licha ya kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi
aliamua kukaa kimya.
Kesi imefunguliwa katika Kituo cha
Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ kwa jalada namba KJN/RB/7122/14
KUJIPATIA PESA KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
No comments:
Post a Comment