Sakata la Kanga Moko Kupigwa Risasi: Mama Mazazi wa Mabinti hao Asimulia mkasa Mzima
Mama mzazi wa binti aliyesababisha wasichana wawili kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya kushiriki ngoma maarufu ya Kanga Moko iliyopigwa marufuku, huko Mwananyamala Kisiwani jijini Dar es Salaam, amefunguka na kusema kuwa hakukuwa na sherehe yoyote nyumbani kwake siku hiyo ya tukio.
Mama huyo, Rehema Aziz alisema waliojeruhiwa walikuwa wakisherehekea
kuolewa kwa mwanaye aitwaye Aziza Aziz, ambao walikuwa ni marafiki zake
na walifanya hivyo kwa mujibu wa mila za watu wa Pwani, za kucheza na
kufurahi wakizunguka mitaani, lakini bila kufanya fujo yoyote.
“Huo ulikuwa ni Mdundiko wa kawaida, tokea zamani tulikuwa hatuombi
kibali na wao walifanya hivyo kama mila zinavyosema, siku ya tukio Juni
18, mwaka huu hatukuwa na sherehe hapa nyumbani isipokuwa jana yake
ndiyo kulikuwa na sherehe ya kumpa zawadi mwanangu.
“Tukio la Juni 18, wasichana ambao ni marafiki zake mwanangu ambaye
kwa sasa yupo kwa mume wake, walikuwa wakisherehekea wenyewe kivyao,
bila mimi kujua, lakini hata hivyo mbona ilikuwa ni mapema mno, saa kumi
jioni na walikuwa ni wanawake tu,” alisema mama huyo.
Kwa upande wake majeruhi Grace Loy (20), mkazi wa Mwananyamala
Mchangani, alisema anachokijua ni kwa alipigwa risasi katika paja la
kulia wakati huo wa vurugu ya kuwataka watawanyike.
“Sisi tulikuwa
tukiwasindikiza watu wa tarumbeta ambao walikuwa wanaume, tuliobaki
tulikuwa wanawake na hakukuwa na vurugu wala hatukumpiga askari ila sisi
tumepigwa risasi kama swala,” alisema Grace.
Majeruhi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zawia Hamis (20),
mkazi Mwananyamala anayedai kupigwa risasi tumboni na kwenye makalio,
alisema ameshangazwa na kitendo hicho.
Walisema ni jambo la ajabu kuwa polisi walitumia nguvu kubwa dhidi ya wanawake waliokuwa hawana silaha yoyote.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Makumbusho, Husna Nondo alisema watu hao
hawakuwa na kibali cha aina yoyote na kusisitiza kuwa serikali
imeshapiga marufuku ngoma za Kanga Moko hivyo amewataka wananchi kufuata
agizo hilo la serikali.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura alipoulizwa
juu ya suala hilo, alisema upelelezi unaendelea ili kubaini tatizo.


No comments:
Post a Comment