Msichana wa kazi ( Hausigeli ) aliyechomwa Pasi na kuteswa kwa miaka mitatu na bosi wake akabidhiwa kwa wanaharakati
Hatimaye Yusta Lucas (20), binti aliyekuwa akiteswa kwa kuchomwa pasi na kung’atwa na mwajiri wake, Amina Maige ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Mwananyamala alikokuwa amelazwa na kukabidhiwa kwa wanaharakati wa Taasisi ya Jipange.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya maridhiano kati ya
Ustawi wa Jamii, mama mzazi wa Yusta, Modesta Simon, Kamati ya Ulinzi na
Usalama Kata ya Makumbusho na Jipange ambao ndiyo iliyofanikisha
kumwokoa binti huyo.
Akizungumza jana, Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Makumbusho, Husna Nondo alisema baada ya kutafakari kwa kina juu ya
usalama na urahisi wa kupatikana pale atakapohitajika, wamekubaliana
binti huyo akae kwa muda kwa mmoja wa wanakikundi kutoka taasisi hiyo.
“Tumeafikiana Yusta aendelee kubaki mikononi mwa
wanaharakati ili iwe rahisi kupatikana atakapohitajika mahakamani, maana
yeye ndiye shahidi wa kwanza. Mama na mjomba wake waliotoka Tabora
wataendelea kukaa Upanga walikofikia,” alisema Nondo.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Hospitali ya
Mwananyamala, Rose Temu alisema wamemkabidhi Yusta kwa Jipange kwa
maandishi na wanaamini yuko katika mikono salama kwa sababu taasisi hiyo
ndiyo iliyokuwa mstari wa mbele kumuokoa.
“Wakati akisubiri kesi yake, tumekubaliana awe
chini ya Jipange tumeona asiendelee kukaa wodini kwan anaweza kupata
ugonjwa mwingine, uamuzi ambao hata mama yake ameuridhia.”
Mwenyekiti wa Jipange, Janet Mawinza alisema
wamekubali kumpokea Yusta kwa ajili ya usalama wake lakini akasema
hataeleza ni wapi atakuwa anaishi kwa kipindi atakachokuwa akisubiri
kesi.
“Sisi tumempokea kama kikundi na tunachoomba ni
vyombo vinavyohusika na suala hili kuhakikisha vinashughulikia suala
lake kwa wakati ili huyu binti aungane na familia yake Tabora,” alisema.
Mama wa binti huyo alisema anaamini binti yake
yuko katika mikono salama. “Hawa Jipange ndiyo walikuwa naye tangu siku
ya kwanza na sioni kama kuna tatizo wao kuendelea kuwa naye.”
Kwa siku tano, Yusta alikuwa amelazwa katika
Hospitali ya Mwananyamala kuuguza majeraha yanayodaiwa kusababishwa na
kung’atwa na kuchomwa na pasi na Maige ambaye alikuwa mwajiri wake huko
Mwananyamala Kwa Manjunju kwa muda wa miaka mitatu.
Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi katika Kituo cha Oysterbay na wakati wowote atafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.



No comments:
Post a Comment