Tuesday, 10 June 2014

AIBU JAMANI..MAMBO YA NDANI YA SHUKA MOKO...MNAFIKI KAA PEMBENI..!



AIBU JAMANI..MAMBO YA NDANI YA SHUKA MOKO...MNAFIKI KAA PEMBENI..!






Hehehe… heeeeee, heiiiya, acha nicheke miye mwana wa marehemu, sijui
wazazi wangu huko waliko wako katika hali gani, nawaombea kwa Mwenyezi
Mungu awape kivuli chake siku ya kiama.




Waweza kuona nacheka ukadhani labda nimejawa na furaha, kumbe nafsi yangu imejaa karaha, imekereheka kama siyo kukereheshwa. 



Kuna watu wengine kwa kweli kila kitu watende wao wakitenda wenzao huwa mwao, hutaka kuicheza ngoma hata kama siyo ya kwao, upo? 



Hivi inaingia akilini mama mtu mzima kutaka kuingilia ndoa ya
mwanaye? Tuchukulie mfano ni wewe mama ungekuwa na mtoto wa kike, ndoa
yake ikawa inaingiliwa na mzazi mwenzako ungefurahi?




Nalisema hili
kwenu nyie wenye tabia hii kwa kuwa huu ndiyo mwarobaini wenye ladha
chungu, lakini ndani yake unapata dawa ya kutibu maradhi yako ya nyongo.


Kwa nini leo nimeamua kuyasema haya? Jamani kuna shoga yangu mmoja
kanijia mikono kichwani machozi churuchuru nikadhani labda amefiwa,
alichonieleza nilibaki mdomo wazi kama siyo kupigwa na bumbuwazi.
 



Eti, mwanaye amekuwa akiendeshwa na mkewe kama gari bovu. Yaani
mkwewe amekuwa ndiye kinara wa nyumba na mtoto wake hafurukuti wala
hatikisiki. 




Kila siku mama anamwambia mwanaye ubaya wa mkewe
lakini mtoto wala hajali, maneno yanaingia sikio hili yanatokea lile,
hasikii kitu juu ya mkewe.
 



Siku moja, shoga yangu akapewa na mwanaye maneno makavu, kuwa hawezi
kuachana na mkewe kama anavyotaka yeye, hilo likamuuma mpaka akaamua
kuja kuniangushia kilio.
 



Mmh, makubwa limao alambe mwingine wewe ukunje uso kama ngozi ya
goti, leo nataka niwaeleze nyie kina mama mnaokosa kazi na kufuatilia
ndoa za watoto wenu, jamani acheniii.
 



Hamuoni aibu, mama mkwe kuacha kazi na kuwa kiguu na njia kufuatilia
ndoa za watoto wenu kama mkia wa ng’ombe. Kwanza kwa mila na desturi za
Kitanzania ni matusi kufanya hivyo.
Mama mtu mzima huna kazi,
unafuatilia nyendo za mkweo, jioni mwanao akirudi unampa  ‘full data’, 
cha ajabu mwanao haoneshi chochote kutokana na  madai yako, unakasirika.
 



Mwanao wa kumzaa mwenyewe akikupuuza unamuona hafai na hana maana,
unaanza kuzunguka mitaani na kusema kuwa, mwanao hajaoa bali kaolewa.
 



Ni jambo la kushangaza kwa mtu mwenye akili zake na aliyedumu katika ndoa kufanya ujinga huo. 



Tunajua kwamba kuna wazazi walioshindwa kuziongoza ndoa zao kwa kukosa
uaminifu, lakini leo ndiyo hao hao wanaokosa uso wa haya na kuanza
kufuatilia maisha ya wakwe zao kisha kupeleka umbeya kwa watoto wao.




Eti, watoto wao wakikataa ushauri wao wanataka kuwatolea radhi, mmh!
Jamani nyie  nani aliwatolea radhi? Mbona yenu mengi tunayajua lakini
hatusemi?




Siye tumenyamaza kwa kuelewa kwamba ndoa ni siri ya watu
wawili, tunafahamu pia kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho wake, kwa nini
tutake kuitwa wachawi kwa jambo ambalo ukweli  unaweza kubainishwa na
mhusika mwenyewe?
 



Heee! Kama mke na mume kuna anayefanya uchafu ni mmoja kati yao ndiye
anayeweza kuubainisha kwa kuwa wote wana macho watayaona na kutoa
hukumu bila kumlaumu mtu yeyote ya nini siye tuyaingilie?
 



Tafadhali, shoga usiwe kimbelembele kama mfuko wa shati kutaka
kuvunja ndoa ya mwanao, unajua mwanao anafanyiwa nini na mkweo? Unajua
analishwa nini? unajua anapumbazwa kwa pumbazo gani? Alaaaa! Acha
ushakunaku.




Wewe kama ungefuatiliwa hivyo ndoa yako ingedumu? Yako ni yako na ya
wenzako pia yako.Napenda kukwambia wewe unayebinua midomo kama samaki
chuchunge na wenzako kuwa msipende kuingilia mambo ya watu wanaojifunika
shuka moja, mtakuja kupatwa na aibu!

Yangu  kwa leo ni hayo, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.

No comments:

Post a Comment