Waziri Tibaijuka Hoi, Venessa Mdee Amsulubu Live Live
Adai anamiliki maelfu ya ardhi hapa nchini Wabunge wamshambulia, Makinda amuokoaCCM waitisha kikao cha dharura kumnusuru
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemlipua Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kwamba anamiliki maelfu
ya ekari za ardhi katika maeneo mbalimbali nchini.
Mdee ambaye ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alirusha
kombora hilo jana bungeni wakati akisoma maoni ya kambi hiyo kwa Wizara
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Makombora hayo ya Mdee, yalimfanya Waziri Tibaijuka, kutumia muda mrefu
zaidi kujibu mashambulizi badala ya hoja za wabunge wakati akihitimisha
hoja yake.
Majibu hayo yalimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kila mara kumtaka
Waziri Tibaijuka ajibu hoja za wabunge badala ya kujikita kumjibu Mdee,
katika masuala yanayoonekana ni binafsi.
Waziri Tibaijuka, alisema kuwa Mdee amekuwa bingwa wa kuiba siri za
serikali ikiwemo mwaka jana kuiba andiko la chuo kikuu na mwaka huu
ameiba barua zake za siri alizomuandikia Waziri Mkuu.
Hoja za-Mdee
Mdee, alisema Waziri Tibaijuka ana maslahi makubwa katika sekta ya ardhi
ambapo anamiliki kiasi kikubwa cha ardhi maeneo ya Kigamboni na Kagera
Wilaya ya Muleba ambako katika eneo la Kyamnyorwa ana hekta 800.
Kwa mujibu wa Mdee, mjini Bukoba, waziri huyo mwenye dhamana ya ardhi, anadaiwa kumiliki ekari 100 alizozipata kiujanja.
Alisema eneo hilo alilipata kwa kuwahamisha wamiliki halali kwa nafasi
yake ya ukurugenzi wa UN-Habitat na baadaye ya uwaziri wa ardhi.
“Mheshimiwa Spika, linapokuja suala la migogoro ya ardhi, Waziri
Tibaijuka anakosa “moral authority” katika kuutafutia ufumbuzi wa haki.
Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliangalia upya
suala lolote la ardhi ambalo waziri atajiingiza kwani nyuma ya sakata
hilo kuna maslahi binafsi yake kama hili la Chasimba, na Kigamboni,”
alisema Mdee.
Mbunge huyo alifichua siri nyingine ya umiliki wa ardhi ya waziri huyo
katika eneo la Kigamboni ambako kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya
na wa kisasa.
Alisema katika eneo hilo, Waziri Tibaijuka, kwenye ekari 50,934
zilizoongezwa kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni,
amejimegea maelfu ya ekari.
Alisema Waziri Tibaijuka aliongeza eneo la mradi kutoka hekta 6,494 zilizokuwepo awali hadi hekari 50,934.
“Hoja hapa ni je kati ya hekta zilizoongezwa 44,440, zinazomilikiwa
binafsi na waziri ni ngapi? Hii haina siri, akikataa kusema wananchi
wanaelewa ni ngapi, na hotuba ya mwaka kesho zitatajwa hapa bungeni,”
alisema Mdee.
Alisema anaitaka serikali kuangalia upya mipango ambayo inatayarishwa na
kusimamiwa na Waziri Tibaijuka na jinsi gani inatekelezwa kwa madai
kuwa haaminiki tena.
Mdee alisema katika migogoro mingi ya ardhi, Waziri Tibaijuka amekuwa
akitajwa kuhusika na katika mazingira hayo ni dhahiri kuna jambo
limejificha, hivyo ni wakati mwafaka kuchukua hatua kabla ya majanga
zaidi kutokea.
Mbunge huyo alimshambulia Tibaijuka, kwamba hawezi kusimamia wizara hiyo
kwani hata kwenye nafasi aliyoachia Umoja wa Mataifa, aliondolewa
kutokana na uwezo mdogo wa kufanya kazi.
Akizungumzia sarakasi za mradi wa Kigamboni, Mdee alisema mpango wa
ujenzi wa mradi huo, umekuwa ukilalamikiwa sana na kutiliwa shaka na-
wananchi wa eneo hilo.
Mbunge huyo alisema mpango huo ambao unaelezwa kuwa wa serikali, sio sahihi kwani umevalishwa koti tu la serikali.
Kwa mujibu wa Mdee, ukweli huo unathibitika kutokana na mvutano uliopo
kati ya wananchi wa Kigamboni wakiongozwa na mbunge, Dk. Faustine
Ndungulile na Waziri Tibaijuka kuhusu kukiukwa kwa sheria ya mipango
miji.
“Huu ni udhaifu mkubwa kwa upande wa utawala kwani ndio kinakuwa chanzo
cha mgogoro usiokwisha na kusababisha hata kama kuna nia njema basi
dhamira ovu inaanza kujitokeza wazi mbele ya uso wa jamii,” alisema.
Mbunge huyo alisema katika kikao cha bajeti mwaka jana, Bunge lilitoa
mwongozo wa kumaliza mgogoro kwa kuitaka serikali kupitia kwa Waziri
Tibaijuka, kukaa na mbunge na wananchi kumaliza mtafaruku huo, lakini
hadi sasa kikao hicho hakijawahi kufanyika.
Kibaya zaidi Mdee alisema wizara imeandaa Master Plan bila
kuwashirikisha wananchi kupata maoni yao kama sheria ya mipango miji
inavyotaka.
“Mheshimiwa Spika, kambi rasmi inauliza je hayo maoni ya mwanzo
yalikusanywa lini? Kama yalikusanywa mbona wananchi wanalalamika?
Tunamtaka waziri atoe majibu ya kueleweka,” alisema Mdee.
Mbunge huyo ambaye jana alikuwa mwiba kwa Waziri Tibaijuka, alihoji kama
kuna uhalali wa kuendelea na mpango huu kabambe pamoja na wakala wa
kuendeleza mji wa Kigamboni.
Mgogoro wa ardhi Chasimba
Akizungumzia mgogoro wa Chasimba, Mdee alisema kwa muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiitwa wavamizi.
Lakini alisema ukweli unabaki kuwa kuna siri kubwa sana iliyojificha ya
namna Kiwanda cha Wazo Hill kwa kutumia viongozi wa kijiji wa kipindi
kuuza ardhi ya wananchi wakiwa ndani, kisha kubadilisha mipaka na
hatimaye kiwanda hicho kupewa hati kinyemela.
Kwa mujibu Mdee, mahakama iliamua- wananchi wahame, lakini pia iliiagiza
serikali kwamba wajibu wake katika mgogoro huu ni kuwapatia makazi
mbadala.
Alisema amri hiyo ilishindwa kutekelezwa kwa madai ya ukosefu wa fedha na eneo la kuwahamishia.
“Mheshimiwa Spika. hatimaye ‘inasemekana’ wizara ilipata ‘eneo’ la ekari
1,000 ukilinganisha na ekari 630 za eneo la Chasimba, mchakato
ulisababisha kuitisha kikao cha wananchi, waziri na timu yake na
mthamini mkuu wa serikali na timu yake, walifikia muafaka wa wananchi
kufanya tahmini na kulipa fidia wote waliotathminiwa ambao jumla yao ni
4096,” alisema.
Mdee alisema wananchi hao waliahidiwa kulipwa sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, pamoja na viwanja mbadala.
“Mheshimiwa Spika, lakini katika kile kilichoonekana kuna harufu ya wizi
na rushwa, katika kikao kilichofanyika baa kikiwahusisha Waziri
Tibaijuka, Diwani wa Kata ya Bunju, Mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya,
pamoja na inayoitwa ‘Kamati ya Wananchi’, wWaziri alisema wananchi
hawatalipwa tena sh 15,000 kwa Square Metre, bali watapewa 5,000 ya
kifuta jasho,” alisema.
Mbunge huyo wa CHADEMA, alisema kilichofanyika baadaye, waziri na timu
yake walianza kutumia vitisho na kuwataka wananchi wafungue akaunti na
kujaza fomu zisizo hata na muhuri wala nembo ya wizara, zikiwataka
waandike namba zao za akaunti na kwamba wangekutana na pesa zao huko
huko.
Na zaidi ya hiyo, wananchi hao waliambiwa asilimia 10 ya pesa
watakayolipwa itakwenda kwenye Saccos, ambayo haijulikani ni ya nani,
imeundwa lini na kwa madhumuni gani.
“Mheshimiwa Spika, mpaka sasa waziri akiulizwa tutajazaje fomu na
kuandika akaunti ili tuingiziwe pesa ambazo hata hatujui ni kiasi gani,
anajibu utakachokikuta hata kama ni 200 ndio halali yako,” alisema Mdee.
Dalili za wizi
Kwa mujibu wa nyaraka- ambazo kambi ya upinzani inazo, Mdee alisema kaya
4,096 zilizofanyiwa tathmini, kwa kiwango cha sh 15,000 kwa mita moja
ya mraba, fedha iliyotakiwa kulipwa ni sh 47,368,357,520/-.
Alisema hiyo inathibitishwa kwa barua ya tarehe 8/11/2013, yenye
kumbukumbu namba CBA 171/312/01 kutoka kwa Waziri Tibaijuka kwenda kwa
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Alisema katika barua husika, pamoja na mambo mengine anampa taarifa
waziri mkuu juu ya uhitaji wa sh 69,051,215,426 kama hitaji la fedha kwa
zoezi zima la kulipa fidia kutwaa eneo la makazi mbadala, kulipanga
eneo jipya kimipango miji, kupima viwanja na kuweka miundombinu ya
msingi hususan barabara, maji, shule ya msingi, dispensari.
Mdee alisema kitendo kinachofanywa na waziri pamoja na uongozi wa
Kiwanda cha saruji cha Wazo kumlazimisha Waziri Mkuu akubali deal hiyo
ifanyike haraka, inatia shaka kwani huenda Waziri Tibaijuka atafaidika
na mpango huo.
Mdee alisema kwa mujibu wa tathmini, kaya zilizofanyiwa tathmini, na
kutakiwa kupewa viwanja mbadala ni 4,096, lakini wizara inataka
kuvilipia viwanja 4,500 na vilivyosalia 404 vya ziada havijulikani ni
mali ya nani.
Taasisi yenye mahusiano na Tibaijuka
Mdee, alizidi kumkaba koo Waziri Tibaijuka kwamba ana mahusiano na
taasisi ya Tanzania Women Land Acces Trust- (TAWLAT) ambayo imo katika
mchakato huu tata.
Alisema kuwa ushahidi unaonyesha kuwa waziri alikishauri kiwanda kuingia
mkataba na taasisi hiyo ya TAWLAT kutoa elimu na kuendesha mazungumzo
na viongozi na wananchi wa Chasimba juu ya mgogoro wao.
Kutokana na mazingira hayo, Mdee alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ina shaka juu ya ushiriki wa shirika hilo katika mgogoro wa
Chasimba pamoja na kazi nyingine za wizara.
Alisema kwenye mgogoro huo wa Chasimba, taasisi hiyo ililipwa sh milioni
300 na milioni nyingine 300 zilizotolewa na Halmashauri ya Kinondoni.
“Mheshimiwa Spika, kwa maelezo ya Waziri Tibaijuka, katika kazi hiyo
taasisi hiyo ililipwa sh milioni 300 na katika mchanganuo niliouainisha
hapo awali, wangelipwa sh milioni 500 kwa kazi hiyo. Nikiwa kama mbunge
wa jimbo husika, nikuhakikishie kwamba hiyo taasisi haikufanya kazi
yoyote,” alisema.
Mdee alisema kazi ya uthamini ilifanikiwa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi
wa Upimaji na Ramani na timu toka Wizara ya Ardhi kuja ofisini kwake
kumuomba awasaidie kutuliza upepo kwani wananchi walikuwa wakiwarushia
mawe.
“Mheshimiwa Spika, ilituchukua mikutano mikubwa si pungufu ya sita mimi
nikiwa msemaji mkuu kuwaelimisha wananchi nia ya tathmini huku wakubwa
hawa wakiwahahakikishia kwamba watalipwa 15,000 kwa square metre na
kupewa maeneo mbadala. Hakukuwa na cha TAWLAT, wala Waziri Tibaijuka,”
alisema.
Kutokana na sarakasi hizo, Mdee alisema kambi ya upinzani inaitaka
Takukuru kufanya uchunguzi wa ushiriki wa TAWLAT kuhusu ushiriki wake wa
shaka katika kazi kadhaa za Wizara ya Ardhi na wasipofanya hivyo,
watawasilisha hoja binafsi- kuhusu sakata hili.
CCM wakutana ghafla
Katika hatua inayohusishwa na ugumu wa bajeti ya wizara hiyo, wabunge wa
CCM walikutana ghafla ambapo pamoja na mambo mengine walijadili
mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo.
Karibu wabunge wote waliochangia bila kujali itikadi, waliishambulia bajeti ya wizara hiyo na kutishia kuondoa shilingi.
Mbali ya wabunge wa CCM kutishia kuondoa shilingi, mawaziri wengi
hawakuwemo wakati Waziri Tibaijuka anasoma bajeti yake na taarifa
zinadai kuwa wamemsusia kwa vile amekuwa hashiriki kwenye bajeti za
wizara nyingine kwa namna yoyote ile.
Mmoja wa wabunge wa CCM, aliliambia gazeti hili kuwa chama kimeweka msimamo wa kumnusuru Waziri Tibaijuka.

No comments:
Post a Comment