Tuesday, 27 May 2014

UKATILI: Baba ampaka mwanae pilipili machoni, amchapa viboko, ngumi na mateke hadi kufa



UKATILI: Baba ampaka mwanae pilipili machoni, amchapa viboko, ngumi na mateke hadi kufa



JESHI la Polisi mkoani Geita, linamshikilia William Kibyala (40), mkazi
wa Kijiji cha Misiri, Kata ya Bugarama, Wilayani Geita kwa kosa la
kumpaka pilipili machoni mwanae John Wiliam (4), na kumchapa viboka
sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa.


 

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Joseph Konyo, amethibitisha Jeshi hilo
kumshikilia mtuhumiwa huyo muda mfupi baada ya tukio hilo lililotokea
Mei 23, 2014 ambapo amesema mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada
ya upelelezi kukamilika.


 

“Mtoto huyu alifariki baada ya kupewa adhabu na Baba yake mzazi kwa
kupigwa na kupakwa pilipili, huyu mtuhumiwa tunamshikilia hadi sasa na
uchunguzi zaidi wa tukio hili bado unaendelea kwahiyo kwa taarifa
nyingine tutawaambia ili muujulishe Umma wa watanzania kupitia kwenu na
vyombo vingine vya habari”
alikaririwa Konyo katika mahojiano na mwandishi wetu


 

Aidha, alisema Baba wa mtoto huyo anadaiwa kufanya ukatili huo baada ya
kumtuhumu mtoto huyo kukataa kumfungulia mlango wakati alipotoka
matembezini usiku wa manane.


 

Baadhi ya wananchi wanaoishi katika Kijiji hicho wamedai kuwa  mtoto huyo alifariki baada ya kuchapwa fimbo mwili mzima, kupigwa ngumi
na mateke, kisha kupewa adhabu ya kukimbia riadha ya kuzunguka nyumba
yao usiku wa manane kabla ya kifo chake.


 

Mmoja wa mashuhuda hao, Irine Kaijage, amesema baada ya mtoto huyo
kumaliza adhabu hiyo alipakwa pilipili machoni na makalioni hali
iliyosababisha mtoto huyo kuzidiwa na kupoteza maisha Mei 24, 2014
jioni.


 

Mmoja wa watoto wa Mzazi huyo, Shija William, alisema mdogo wao alikuwa
akipewa adhabu hiyo mara kwa mara na Baba yao kwa madai kwamba Mama yao
alimbambikizia mdogo wao kwani yeye hakumzaa.

No comments:

Post a Comment