UHUSIANO WA TANZANIA NA UINGEREZA SHAKANI WAZIRI AMSHUSHIA TUHUMA NZITO BAROZI WA UINGEREZA
Kauli ya Waziri ni kauli ya Serikali.Tuhuma dhidi ya Balozi wa Uingereza ni Tuhuma dhidi ya Serikali na Taifa la Uingereza
Naibu waziri wa Nishati na Madini Mh.Steven Masele ametoa tuhuma nzito
bungeni akimuhusisha balozi wa Uingereza nchini kwa tuhuma za Rushwa
kuhusiana na sakata la IPTL na pia kufanya ujasusi na kudai kuwa balozi
anatakiwa kuchukuliwa hatua huku akimtaka akajieleze wizara ya mambo ya
nje.
Hizi ni tuhuma nzito kabisa na ujasusi ni kinyume cha sheria za nchi na
sheria za kimataifa.Waziri Masele amewatangazia Watanzania na Dunia kuwa
Uingereza sio nchi rafiki kwa Tanzania na ni adui mkubwa anayehujumu
uchumi wa nchi yetu.
Ni kinyume na kifungu namba 6 cha sheria ya kuzuia Rushwa sura ya 329
iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002 ikisomwa pamoja na aya ya 1 jedwali la
kwanza ikisomwa na aya vifungu 57(1) na 60 vyote vya uhujumu uchumi na
uhalifu uliopangwa sura ya 200(Iliyofanyiwa Mapitio mwaka 2002).
Mkataba wa kimataifa Vienna unaoshughulikia muhusiano ya kidiplomasia wa
Mwaka 1961(Vienna convention on diplomatic relations 1961) katika ibara
ya 41(1) unakataza mabalozi na wanadiplomasia kuingilia masuala ya
ndani ya nchi wenyeji na pia kutimiza wajibu wa kuheshimu kinga ya
kidiplomasia .
Tuhuma za ujasusi na Rushwa ni tuhuma nzito zinazokiuka ibara hii na pia zinavunja sheria za nchi mwenyeji(Host Country) .
Ni makosa ya jinai kujihusisha na utoaji na upokeaji wa Rushwa na mbaya
zaidi kufanya ujasusi. Ibara ya 29 ya mkataba huo huo wa Vienna inatoa
kinga kwa wanadiplomasia kushotakiwa kwa kesi za kiraia au za
jinai(Immune from Civil and Criminal Prosecution) labda kama ibara ya 32
ya mkataba huo huo itatumika kumuondolea kinga.
Anachosema Waziri Masele ni kuwa Balozi wa Uingereza anastahili
kufukuzwa nchini kwa kutumia ibara ya 9 ya mkataba huo huo wa Vienna na
kumtangaza kuwa ni mtu asiyetakiwa nchini (Persona non grata)? Uingereza
ni wahisani wakubwa wa bajeti ya nchi yetu na pia ni wafadhili wa mradi
wa umeme vijijini REA ambako wamechangia Paundi 71 Milioni.
Ni lazima ufisadi wa IPTL uwaguse maana Uingereza wanatumia fedha za
walipa kodi wao kuifadhili serikali ambako Mafisadi wamekwapua kwa
maslahi binafsi. Pia benki ya Standard Chartered ni Benki ya Uingereza
na ni wajibu wa Balozi katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi
kufuatilia kwa karibu sakata hili.Kazi ya Balozi ni kufuatilia na
kuhamasisha au kutoa msaada kwa makampuni na wafanyabiashara kutoka nchi
yake wanapokua na changamoto bila kuvunja sheria za nchi husika au
sheria za kimataifa.
Ni jambo la ajabu kuwa Waziri anatoa tuhuma Bungeni na kumuamuru Balozi
akajieleze wizara ya mambo ya nje.Wizara ya Mambo ya nje kupitia
mwanadiplomasia mkuu (Top Diplomat) ambaye ni waziri wa Mambo ya Nje
ndiye aliyetakiwa kufanya mashauriano na Balozi kuhusu tuhuma hizo na
sio kauli za kihuni zinazoweza kuharibu mahusiano ya kihistoria kati ya
Uingereza na Tanzania.
Miaka Michache iliyopita Uingereza kupitia shirika la SFO waliweza
kuthibitisha nia njema kwa Tanzania katika kulinda raslimali zetu kuliko
tunavyoweza kuzilinda wenyewe kwa kupigania na kurudisha mabilioni ya
fedha yaliyoibiwa wakati wa ununuzi wa Rada ya Kijeshi,shukrani kwa
Bi.Claire Short aliyesimama kidete kuhakikisha Fedha za walipa kodi wa
Tanzania maskini zinarudishwa nchini wakati ambao viongozi wetu
tuliowachagua walionekana kutokua na moyo wala ari ya kushughulikia
Tatizo hilo.
Sasa natoa Rai kwa Waziri wa Mambo ya Nje Mhe.Bernard Membe atoe Msimamo
wa Serikali kuhusu tuhuma hizi za kushtua na zinazoweza kuharibu
mahusiano ya kihistoria kati ya wananchi wa Tanzania na Uingereza.Ni
tuhuma nzito za aibu.
No comments:
Post a Comment