Bunge la Bajeti kuongezewa muda....Lengo ni kujadili migogoro ya wafugaji na wakulima, pia kujadili muswada wa misamaha ya kodi
MKUTANO wa 15 wa Bunge la Bajeti uliopangwa kumalizika Juni 27, mwaka huu, sasa utaongezewa muda kuruhusu Muswada wa Serikali na Azimio la Bunge juu ya migogoro ya wafugaji na wakulima. Kabla ya kuahirisha kikao cha juzi, Spika wa Bunge, Anne Makinda alieleza kuwa upo uwezekano huo wa Bunge kusogezwa mbele zaidi.
Alisema
hiyo inatokana na taarifa alizonazo kuwa Serikali inataka kuwasilisha
Muswada kuhusu Misamaha ya Kodi na kuwapo kwa Azimio la Bunge kuhusu
migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.
“Tutaongeza
siku baada ya bajeti, kwani kwa taarifa nilizonazo Serikali inataka
kuleta Muswada kuhusu VAT katika Misamaha ya Kodi,” alisema Makinda.
“Kuna
mtu alisema hapa, sijui mimi nakwamisha nini…sihusiki mimi, hili ni la
Serikali. Pia msisahau kuna Azimio la Bunge kuhusu migogoro ya wakulima
na wafugaji,” aliongeza.
Wiki
iliyopita, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema iwapo Muswada
wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hautapelekwa bungeni, atakusanya
saini za wabunge kumwondoa Spika madarakani.
Lugola
aliyasema hayo alipoomba Mwongozo wa Spika, ambaye wakati huo hakuwa
Makinda katika kiti chake, akitaka kufahamu ni lini muswada huo
unaolenga kufuta misamaha ya kodi, utapelekwa bungeni.
Alisema
amepata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali ya Mitaa, Rajab Mbarouk Mohamed ambaye ni Mjumbe
wa Kamati ya Uongozi kuwa kamati hiyo iliiagiza Serikali kuwasilisha
haraka Muswada wa VAT.
Alisema
lengo la kutaka muswada huo bungeni ni kupitia na kufuta misamaha yote
ya kodi isiyo na tija. Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2012/13 inaonesha ipo misamaha ya
kodi ya Sh trilioni 1.5. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Serikali
ndiyo iliomba kuleta Muswada wa VAT katika Bunge hili la Bajeti.
Kuhusu
migogoro ya wakulima na wafugaji, Bunge liliagiza Kamati ya Kudumu ya
Maji, Kilimo na Mifugo chini ya uenyekiti wa Profesa Peter Msolla,
kuangalia suala hilo na kupeleka mapendekezo yake ya jinsi ya kumaliza
tatizo hilo linaloshika kasi nchini.
Bunge
la Bajeti kwa kawaida huwa halina miswada, kwani wabunge hujikita
katika kujadili bajeti za wizara mbalimbali pamoja na Bajeti Kuu ya
Serikali.
Mkutano wa sasa ulianza Mei 5, mwaka huu na ulipangwa kumalizika Juni 27, mwaka huu.
Jana,
ilikuwa zamu ya wizara za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja
na Nishati na Madini ambayo mjadala wake unaendelea leo. Kesho, Waziri
wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa
atawasilisha bajeti yake asubuhi na jioni itasomwa ya Wizara ya Maji ya
Profesa Jumanne Maghembe.
Kwa
mujibu wa ratiba, Jumatatu utaendelea mjadala wa Wizara ya Maji, kabla
ya kumalizia bajeti za kisekta kwa kuwasilishwa Bajeti ya Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Jumanne ijayo na kufuatiwa na Wizara ya Fedha siku
inayofuata.
Kuanzia
Juni 5 hadi 11, mwaka huu, zitatumika kwa Serikali kushauriana na
Kamati ya Bajeti kufanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa
taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara.
Pia
kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe watakaowakilisha Bunge katika
taasisi/vyuo mbalimbali na shughuli nyingine yoyote kwa maelekezo ya
Spika.
Juni
12, itakuwa siku ya Bajeti ambapo asubuhi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira atawasilisha Taarifa ya Hali
ya Uchumi nchini.
Kuanzia
Ijumaa ya Juni 13, wabunge watasoma na kutafakari Bajeti ya Serikali
kabla ya kuanza mjadala wa siku saba kuanzia Juni 16 hadi Juni 24, mwaka
huu.
Juni
25, itasomwa miswada miwili, Muswada wa Sheria Mbalimbali na Muswada wa
Fedha ambao utasomwa kwa mara ya tatu Juni 27, ambayo ilipangwa iwe
siku ya kuhitimisha Mkutano wa Bunge la Bajeti.
Credit >>Habari Leo
Credit >>Habari Leo

No comments:
Post a Comment