Thursday, 28 November 2013

Uanachama wa Zitto Changamoto Ndani ya CHADEMA....Wasira adai dhambi ya Ukabila Itakimaliza Chama Hicho...!!


UANACHAMA wa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Zitto Kabwe umetajwa kuwa ‘kaa la moto’ kwa
uongozi wa chama hicho hata kabla ya kiongozi huyo
kujibu mashitaka 11 yanayomkabili ili kunusuru
uanachama wake.
Duru za siasa ndani ya chama hicho, zinasema Chadema
haiko tayari kukabiliana na mtikisiko wa Zitto kuvuliwa
uanachama, kwa kuwa hatua ya kuvuliwa madaraka tayari
imegharimu umoja na utulivu wa chama hicho.
Taarifa hizo zinasema kwa sasa kuanzia Kamati Kuu
mpaka wanachama, kuna mpasuko mkubwa ambao namna
pekee ya kuuziba ni kumshawishi Zitto na Mwenyekiti
Freeman Mbowe, kupatana.
Hata hivyo, wakati jitihada za kuwapatanisha zikiendelea,
duru za siasa zinaeleza kuwa kambi ya Mbowe ina
wajumbe wanaoshinikiza kumtosa Zitto na kuwa tayari
kukabiliana na gharama zake.
Majimbo
Mtoa habari wetu kutoka ndani ya Chadema anaeleza kuwa
hofu kubwa iliyopo kama Zitto atanyang’anywa
uanachama, ni ukweli kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa
2015, wanaweza kupoteza majimbo mengi na kuipa
mwanya CCM kupita kirahisi.
“Ni kweli huu si mgogoro wa kwanza kwa Chadema na
mara zote viongozi walipovuliwa madaraka kulitokea
mtikisiko, lakini si kama huu wa Zitto… mbaya zaidi,
majimbo ya viongozi tuliowavua madaraka leo hii
yamepokwa na CCM, hatuko tayari kupoteza zaidi,”
alisema mtoa habari huyo ambaye hakuwa tayari kutajwa
jina.
Akitoa mfano, alisema mgogoro kati ya Chadema na Katibu
Mkuu wa zamani Dk Aman Kabourou, ndio ulisababisha
jimbo la Kigoma Mjini lililokuwa moja ya majimbo ya
Chadema, leo hii kukaliwa na CCM.
Mbali na Kigoma Mjini, mtoa habari huyo alikumbushia pia
jimbo la Tarime, alikokuwa Makamu Mwenyekiti, Chacha
Wangwe, ambalo mbali na kushinda katika uchaguzi
mdogo baada ya kifo chake, leo linashikiliwa na CCM.
“Unajua hata kwa Zitto (Kigoma Kaskazini) ukiangalia
kama kweli tukimtosa, sina hakika kama tutarejesha lile
jimbo. Na hata kwa Arfi (Said, Makamu Mwenyekiti
aliyejiuzulu, Mbunge wa Mpanda Kati), kama yule mzee
tukimchezea hatuna chetu,” alisema.
Alipoulizwa afafanue kuhusu mpasuko huo, alikataa na
kuhoji: “Kwani wewe huoni, mbona wenzenu wameandika
mpasuko uliotokea katika Kamati Kuu?”
Mbali na mtoa habari huyo, hata katika waraka unaodaiwa
kusababisha mtafaruku huo ambao Dk Kitilla Mkumbo
alikiri kuuandaa, Chadema imetajwa kuwa na udhaifu wa
kushinda majimbo katika uchaguzi mdogo.
“Tangu uongozi huu uingie madarakani, kumefanyika
uchaguzi mdogo mara nane, lakini tumeshinda mara mbili
tu sawa na asilimia 25,” alisema Dk Mkumbo katika
waraka wake.
Usuluhishi
Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
kutangaza kumwandikia Zitto mashitaka yake na kumpa
siku 14 za kujibu, tayari kumeripotiwa kuwa nyuma ya
pazia chama hicho kimeamua kumwangukia Zitto yaishe,
ikiwa ni pamoja na kumwahidi cheo kikubwa kuliko Naibu
Katibu Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo katika uchaguzi mkuu wa
Chadema Juni mwakani, Zitto atashawishiwa kugombea
nafasi ya Makamu Mwenyekiti bila mpinzani au na
mpinzani dhaifu na Mbowe ataachiwa kugombea uenyekiti
bila mpinzani au na mpinzani dhaifu, lengo likiwa
kurejesha umoja wakati wakijiandaa na Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Pia inadaiwa Zitto ataahidiwa kupewa fursa ya kugombea
urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Wasira
Akizungumzia mgogoro huo akiwa mkoani Kagera, Mjumbe
wa Kamati Kuu ya CCM, Stephen Wasira, alisema anajivuna
kwamba ndani ya chama chake hakuna ubaguzi kama
ilivyo katika vyama vingine vya upinzani a mbavyo alidai
kiongozi wa ngazi ya juu lazima atoke kabila fulani.
Alidai katika baadhi ya vyama, ikitokea mtu ametoka kabila
tofauti akataka kugombea uongozi ngazi ya juu, kunazuka
vurugu na kufukuzana kwa visingizio vya kuvunja katiba za
vyama hivyo.
“Mara nyingi huwa natumia kauli ya Mwalimu Julius
Nyerere kuwa ubaguzi ni sawa na kula nyama ya mtu,
ukiishaionja huiachi kwa hiyo wameionja inawatafuna.
“CCM hatuna sababu ya kushangilia matatizo yao na
hatuwaogopi wala hatutaki upinzani ufe, kwa sababu
upinzani ni mfumo ulio ndani ya nchi, ila nasi tuache
makundi yanayotokana na uchaguzi, ili tuendelee kushika
Dola kama ilivyo ada yetu,” alisema Wasira.
Vyuo vikuu
Baadhi ya wanachama wa Chadema, wakiwamo wanafunzi
wa vyuo vikuu, walikutana Dar es Salaam jana na
kutangaza mgogoro wa kiutawala kati ya wapigania
demokrasia ndani ya chama hicho na wahafidhina.
Wanachama hao waasi ambao walisema ni wapigania
demokrasia ndani ya chama hicho; lakini kwa tafsiri ya
viongozi wa Chadema ni ‘wahaini’, wametangaza
kuzunguka nchi nzima kuhamasisha wanachama wa
chama hicho wakatae baadhi ya watu waliopandikizwa
kwa kukaimishwa nafasi za uenyekiti kwa manufaa ya
wahafidhina.
Baadhi ya wanachama hao wakiongozwa na Greyson
Nyakarungu, walidai wanatambua kuwa mgogoro ndani ya
Chadema umetokana na Mwenyekiti Mbowe kutamani
kuendelea kuongoza chama kwa gharama yoyote.
Nyakarungu alidai Mbowe anatamani aendelee kutawala
hivyo kuzunguka katika baadhi ya mikoa na kuwaondoa
katika nafasi zao viongozi waliochaguliwa kidemokrasia,
ambao wanaonekana kutomwunga mkono kwa kisingizio
cha kutowajibika.
Nyakarungu ambaye alijiita Brigedia wa Uasi huo, alisema
watu wote waliopenyezwa kukaimu nafasi hizo za uongozi
mikoani wajiondoe haraka “kabla hatujawaondoa kwa
nguvu.
“Sisi tumeamua kama tulivyozunguka nchi nzima na
kampeni ya Washa Taa Mchana, tutazunguka nchi nzima
kuwaambia wanachama ubovu huu wa wahafidhina.
“Tunamwonya Zitto na Dk Mkumbo tabia zao za kusema
kuwa wanaheshimu uamuzi wa CC huku wakijua ni nini
kitatokea, waache mara moja, kwani unyonge wa aina hii ni
kuendelea kuruhusu baadhi ya watu kupora rasilimali za
chama,” alidai Nyakarungu.
Nyakarungu, Jeremia Fumbe wa Chuo Kikuu cha Ardhi na
Likapo Bakari ambaye alifukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma,
walisema wao ni majeruhi wa kufinyangwa kwa
demokrasia ndani ya chama hicho, na kila hoja ambayo
wanatoa wamekuwa wanaitwa masalia ya Zitto.
Nyakarungu alisema watu wote wanaoitwa wasaliti ndani
ya chama hicho au ‘wanaotumwa na CCM’ hoja yao
imekuwa moja tu ya matumizi ya fedha za chama hicho,
hoja ambayo pia walidai imemgharimu Zitto.
“Tunafikia hatua wahafidhina wanasema wazi kuwa ni
bora chama kishuke daraja kuliko kupewa mtu wa nje, mtu
wa kuja, mtu wasiyemfahamu,” alisema Nyakarungu na
kusisitiza kuwa wanachama wa Chadema kutoka Mara na
Kigoma ndio wamekuwa wahanga zaidi.
Nyakarungu, ambaye alidai alijiunga na chama hicho
mwaka 2005 na kushiriki kujenga, alisema kilichomponza
Zitto ndani ya chama hicho ni kuhoji matumizi ya chama
hicho kupitia kamati ya Bunge ya PAC, ndio maana
alishambuliwa yeye binafsi wakati huo ulikuwa uamuzi wa
Kamati ya Bunge.
“Viongozi wetu wa Chadema wanahoji Serikali na matumizi
ya fedha za walipa kodi wakitaka uwazi na usawa, leo
wanataka kutonywa mapema ili wafanye marekebisho ya
kuficha uovu wa matumizi ya pesa? “Zitto kama kiongozi
anayejipambanua asingeweza kuwatonya ili wafiche uchafu
katika matumizi ya fedha huku akitengeneza nafasi ya
kuumiza vyama vingine, hii ni dalili ya udikteta. Na kwa
kuwa aligusa mkia wa mfalme nge ni lazima ang’atwe,”
alidai Nyakarungu.
-Habari leo

No comments:

Post a Comment