Thursday, 28 November 2013

MWIGAMBA:SITOKI CHADEMA NA WALA SIOMBI RADHI -ATOA UFAFANUZI KUHUSU WARAKA WA MKAKATI WA MABADILIKO 2013 TAARIFA YA SAMSON MWIGAMBA KWA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU WARAKA WA MKAKATI WA MABADILIKO 2013


Jumatano, 27 Novemba 2013
Jana katika taarifa kwa waandishi wa habari, Mhe.
Tundu Lissu na Mhe. John Mnyika waliudanganya
umma kuhusu waraka unaohusu Mkakati wa
Mabadiliko 2013. Katika maelezo yao
waheshimiwa hawa, pamoja na mambo mengine,
walidai kuwa waraka uliosambazwa kwenye
vyombo mbalimbali vya habari ni feki. Ukweli ni
kwamba:
Ninathibitisha kwamba waraka uliosambazwa
kwenye vyombo mbalimbali vya habari na
mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno kama
nilivyousoma katika magazeti ya HabariLeo,
Jamhuri na Rai, pamoja na nakala iliyopo Jamii
Forum. Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndio
wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye
kompyuta mpakato (laptop) yangu ambako ndiko
ulikoibwa na viongozi wa chama baada ya
kunipora kwa nguvu laptop yangu Oktoba 25 na
kukaa nayo hadi jioni ya Oktoba 28. Naomba kila
mtu asome neno kwa neno waraka ninaowapa leo
halafu afananishe na ule uliopo kwenye magazeti
na kwenye mtandao ili mjiridhishe kama kweli sio
wenyewe. Kama Lissu na wenzake wana mpango
wa kuuchakachua waraka huu wamekwama!
Waraka huu si wa uhaini wala mapinduzi wala
usaliti kama inavyodaiwa na akina Lissu. Huu ni
waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali
ndani ya chama ambao ulikuwa ufanyike Desemba
2013, na ambao sasa umesogezwa mbele.
Napenda ijulikane kwamba wakati wa uchaguzi si
jambo la ajabu kuwa kwa wanachama kuwaunga
mkono wagombea tofauti. Nimekuwa karibu na
Mwenyekiti Mbowe kwa miaka mingi na ninajua
kwamba yeye naye anao mkakati tena
unaohusisha mbinu haramu za kuhakikisha
anammaliza Zitto na yeye kupita bila kupingwa
kwenye uchaguzi huo. Wanaoshiriki mkakati wake
ni pamoja na Lema, Lissu na wakurugenzi kadhaa
waliopo makao makuu.
Waraka huu ulipaswa kuwa siri ndani ya watu
watatu tu (M1, M2 na M3) na haikutarajiwa
kwamba ungevuja kwa jamii. Bahati mbaya
viongozi wa chama baada ya kuunasa waraka huu
kutoka kwenye komputa yangu mpakato (laptop),
na baada ya kikao cha Kamati Kuu, waliamua, kwa
jazba na bila kutumia busara ya kiuongozi,
kuusambaza waraka huo kwenye vyombo vya
habari kwa lengo la kuwakomoa na kuwadhalilisha
waandaji. Sasa baaada ya kugundua madhara ya
waraka huo machoni pa jamii wameamua kuukana.
Ni ajabu kwamba wanaukana waraka ambao
waliusambaza wenyewe.
Nasisitiza kwamba mambo yaliyopo kwenye
waraka ni bayana na dhahiri. Sibahatishi kwa
sababu mimi nimefanya kazi makao makuu kama
Mhasibu Mkuu hadi Mwezi Aprili 2012. Ni kwa
kutambua uozo uliopo katika uongozi wa chama
makao makuu niliona umuhimu wa kubadilisha
uongozi kwa njia za kidemokrasia ili tukiokoe
chama na hatukuwa na nia wala sababu za
kuanika haya yote kwenye umma. Kwa sababu za
chuki na kukosa busara za kiuongozi huyo
anayeitwa Mwanasheria Mkuu akawashauri
viongozi wetu kijinga wauanike waraka mbele ya
macho ya watanzania. Wangekuwa na akili na
busara baada ya yote haya kutokea wangejiuzulu
au kuitisha uchaguzi mara moja.
Tunatambua kwamba viongozi wetu wanamchukia
Mheshimiwa Zitto Kabwe kwa siku nyingi sana na
wametamani kumfukuza siku nyingi. Hata hivyo,
ninawashauri watafute sababu nzuri za kumfukuza
uongozi na hata uanachama kwa sababu yeye
hahusiki na waraka wetu wa Mkakati wa
Mabadiliko 2013 hata chembe, pamoja na kwamba
yeye ndiye alikuwa na bado ndiye mlengwa mkuu,
kama atakubali.

No comments:

Post a Comment