Thursday, 28 November 2013

JB: MLOKOLE MWENYE KICHAA CHA MUZIKI


AKISIKIA muziki unapigwa mahali fulani vinyweleo
humsisimka, kichwa hutingishika na kama yuko
mahali ambako anaweza kujiachia basi lazima
aingie kati kuchangamsha mwili kwa kusakata
rhumba.
Haijalishi ni muziki wa aina gani unapigwa wakati
huo isipokuwa anachoangalia ni mazingira tu.
Ukimpigia Bolingo, R&B, Country, Bongo Fleva zote
zitamkuna. Yote kwa yote mwanamuziki
anayeikonga roho ya JB duniani kote ni Don
Williams.
“Ninapenda kusikiliza na kucheza muziki, lakini
inategemea wakati huo nipo kama nani, nikiwa
kama JB yaani mwigizaji kuna aina ya muziki
huwa napendelea halikadhalika nikiwa Jacob,”
anasema JB.
Anasema kutokana na kazi yake amejikuta akizijua
aina nyingi za muziki na kujiongezea orodha ya
nyimbo katika maktaba yake, lakini hii
haijambadilisha kuwa yule mtu wa kawaida
mwenye chaguo la kipekee.
“Unaniona kwenye majukwaa ya muziki, kumbi za
starehe na kwingineko nikijirusha vilivyo, lakini
huyo ni JB na si Jacob, Jacob anaenda kanisani na
kucheza nyimbo za Injili,” anasema JB.
JB anasema yeye ni mlokole, hivyo katika maisha
ya kawaida hupendelea kusikiliza nyimbo za Injili
kwa kuwa ndivyo imani yake inavyomruhusu.
“Nimeokoka, mara nyingi huwa ninasikiliza nyimbo
za Injili, lakini kwa sababu ninapenda aina
nyingine ya muziki huwa ninasikiliza zile ambazo
zina mafundisho,” anasema JB.
Anasema mbali na kusikiliza nyimbo za Injili, huwa
anapenda kuwasikiliza wanamuziki kama Jose
Chameleon, Ben Pol, Profesa Jay, Lady Jay Dee,
Twanga Pepeta na wengineo wa nyimbo za
kidunia.
“Ninapenda sana muziki, maisha yangu
yametawaliwa na kusikiliza au hata kucheza pale
ninapopata nafasi iwe nyumbani, kanisani hata
kwenye hadhira,” anasema.
Anasema pamoja na kuwa huonekana katika kumbi
za starehe na klabu za usiku, haimaanishi kuwa
anakwenda huko kucheza muziki bali hufanya
hivyo kujifunza mambo mbalimbali.
“Kama utakumbuka kabla ya kutengeneza filamu
yangu ya ‘Senior Bachelor’, nilikuwa naenda sana
klabu, sikwenda kule kufuata muziki ingawa
kiukweli nilikuwa nafurahia, lengo langu lilikuwa
kujifunza namna mapedeshee na madj
wanavyojirusha ili niweze kuicheza nafasi hiyo
vizuri,” anasema JB.
Akizungumzia ujio wake mpya katika filamu,
mwigizaji huyo amesema yupo mbioni kuachia kazi
mfululizo huku akisisitiza kuwa filamu yake mpya
aliyoshirikisha mwanamitindo, Jokate Mwegelo,
itatoka baada ya miezi sita.
“Napigiwa simu nyingi, kila mtu anataka kuiona
filamu aliyocheza Jokate, lakini siwezi kuitoa
mpaka mwezi wa nne mwakani kwani nina kazi
nyingi ambazo inabidi zitoke kwanza,” anasema.
Akizungumzia sababu za kumshirikisha Jokate
katika filamu hiyo iliyopewa jina la ‘Mikono
Salama’, anasema ni kutokana na umbo lake
ambalo lilionekana kuwa lingefaa katika nafasi
hiyo.
“Unajua Jokate ana kaumbo fulani kazuri ambako
unaweza kukachezesha nafasi yoyote, wasanii
wengi wamezeeka kuna nafasi huwezi
kuwachezesha tena,” anamalizia.
-Mwanaspot

No comments:

Post a Comment