Wednesday, 27 November 2013

DIAMOND BAADA YA KUTANGAZA AJIRA SASA ATANGAZA DEMU ANAYEMPENDA JE WAMJUA?


UKIFIKA katika mtaa anaoishi mwanamuziki Diamond
maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam utaanza kuhisi
kuwa kuna staa anayeishi maeneo hayo, macho ya wengi
huanza kumtazama mtu anayeelekea katika geti la nyumba
anayoishi msanii huyo. (HM)
Muda wote geti hilo limefungwa. Ili uweze kuingia ndani
itakulazimu ubonyeze kengele itakayoashiria kuwa kuna
mgeni nje anahitaji kuingia ndani. Hata hivyo hauwezi
kupenya kirahisi ndani hadi uulizwe shida yako na kama
hauna miadi na mtu yeyote anayeishi ndani ya nyumba hiyo
haitakuwa rahisi kuingia.
Mwanaspoti lilitinga katika nyumba ya msanii huyo
na kushuhudia ukimya wa hali ya juu ilhali kuna watu
ndani. Baada ya kufunguliwa geti tuliingia ndani na
kupokewa na Diamond aliyekuwa ameketi katika sebule
iliyonakshiwa na mapambo makini ukutani huku ikiwa na
samani chache lakini za gharama kubwa.
Tulitumia saa mbili mfululizo katika mahojiano na Diamond
ambaye alifunguka kwa kila swali aliloulizwa na kujibu kwa
ufasaha na ufafanuzi mpana.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje katika muziki?
Diamond: Nina mipango makini katika kazi zangu. Mambo
yote lazima yapitie kwa meneja wangu ndipo yanifikie
mimi, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza na mimi moja
kwa moja lazima apite huko na hiyo ndiyo staili ya
Diamond. Nimejipanga kuhakikisha nafanya kazi gani, kwa
wakati gani na sikurupuki tu, japo katika utengenezaji wa
nyimbo zangu naweza nikapata wazo basi hapo hapo
nikatengeneza mistari.
Mwanaspoti: Utendaji kazi wako ukoje kuanzia asubuhi
hadi jioni?
Diamond: Saa tano asubuhi, nikishaamka kitu cha kwanza
ni kwenda 'gym', mara nyingi ni hapa nyumbani kama
unavyoona hapo nje kuna sehemu ya mazoezi na sehemu
nyingine zilizopo ndani, mara nyingi hutumia muda wa saa
moja. Ifikapo saa sita na nusu huwa naanza kufanya kazi
zangu lakini itategemea na ratiba zangu za siku ambazo
ndio mwongozo wangu wa kuimaliza siku. Baada ya hapo
napumzika kwa muda fulani na baadaye jioni huendelea na
kazi na mara nyingi kazi zangu huwa nazimaliza usiku wa
manane.
Mwanaspoti: Unalala saa ngapi? Na unalala kwa muda
gani?
Diamond: Muda wangu wa kulala mara nyingi ni saa kumi
na moja alfajiri na kama sikuwa na kazi nyingi studio basi
nitalala saa nane usiku. Muda wangu wa kulala ni saa sita
mpaka nane kwa siku. Ila hata kama nikilala mapema
kuamka ni saa tano asubuhi ila itategemea na nini
ninakifanya siku inayofuata na kama nina kazi maalumu na
ya mapema itanilazimu niamke mapema ili kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Shughuli gani zinazokuchelewesha mara kwa
mara kulala?
Diamond: Ni kurekodi na wakati mwingine shoo. Kwa wiki
ninafanya shoo nyingi, kama ni tatu basi siku zote tatu
nitalala alfajiri. Siku nyingine zinazosalia ninalala usiku wa
manane kwa kuwa huwa nakuwa studio na sehemu
nyingine ambazo hunilazimu kufanya kazi kwa kipindi
kirefu usiku.
Mwanaspoti: Kati ya usiku na mchana ni muda upi
unaopenda kurekodi?
Diamond: Kazi zangu narekodi usiku na ndiyo muda
ninaopendelea zaidi. Mara nyingi napenda kurekodi saa 7
usiku ili niwe na muda na saa nyingine ni kuepuka lawama
kurekodi mchana, kwasababu vijana wengi chipukizi
wataona napendelewa. Unajua ninapoingia studio napenda
kufanya kazi kwa muda mrefu, hata hivyo iliyo bora sifanyi
bora liende na siwezi kufanya kazi na prodyuza
anayenipeleka tu, ni lazima na mimi nipime kama kazi
niliyoifanya inakwenda vile ninavyotaka au kama yeye
anavyotaka ilimradi tufanye kazi nzuri na iliyo
bora.
Mwanaspoti: Unatumia muda gani kurekodi singo moja na
kwa upande wa video ni siku ngapi?
Diamond: Inategemea, inaweza kuwa siku mbili au miezi
sita lakini nyimbo nyingi zinatumia muda mwingi
kwasababu wakati mwingine naanza halafu napata shoo
hivyo inanibidi nipange muda mwingine wa kurekodi. Kuna
nyimbo zangu ambazo nilizifanya kwa muda mrefu sana
hizo huwa sizisahau ikiwemo Ukimwona, Mbagala, Nataka
Kulewa na nyinginezo. Nakumbuka katika kazi nilizofanya
kwa muda mfupi ni My Number One nilioufanya kwa
prodyuza Sheddy Clever kwa kipindi kifupi sana pamoja na
Mapenzi Basi sambamba na Binadamu hizi ni baadhi ya
kazi ambazo hazikunipasua sana kichwa kuzikamilisha.
Mwanaspoti: Una prodyuza wako maalumu au studio yako
mwenyewe?
Diamond: Sina prodyuza maalumu kila kazi nitakayotaka
kuifanya ninatafuta prodyuza yule ninayemtaka hata kama
sijawahi kufanya naye kazi. Ninafanya hivi nikiwa na
malengo maalumu kwa kujiweka vizuri mimi kama msanii
na hata kuwapa nafasi maprodyuza mbalimbali kutia
mkono kwenye kazi ya mikono yangu. Ninaogopa kuwa na
prodyuza maalumu kwa kuwa najua atanisumbua ikiwa
atajua kwamba namtegemea yeye pekee katika kazi zangu.
Studio sina kwa sasa ila nina mikakati ya kuwa na studio
kwani nimeshanunua baadhi ya vifaa.
Mwanaspoti: Unadhani ndiyo sababu iliyokufanya
ukagombana na Bob Junior au Manecky?
Diamond: Hapana haya mambo yalishapita lakini nilijifunza
mengi ndiyo maana niliamua kuja na staili hii. Naogopa
kubaki kuwa msanii ninayetegemea prodyuza fulani, bila
yeye siwezi kufanya muziki, lakini mimi ni Diamond
ninaweza kufanya muziki na prodyuza yeyote naye
akaonyesha ufundi wake kupitia kazi yangu.
Mwanaspoti: Shoo gani kubwa kuliko zote uliyowahi
kufanya ambayo haijawahi kujirudia?
Diamond: Diamond Forever. Hii ilikuwa kubwa sana
ambayo sitakaa nikaisahau, ilihudhuriwa na watu wakubwa
na maarufu hapa nchini hata hivyo ilikuwa ya kipekee
ambayo haijafanana na yoyote ile. Ya pili ni ile ya Dar Live
ambayo nilifanya baada ya kushuka katika helikopta ile pia
ilikuwa kubwa. Lakini kwa nje ya nchi ni Mombasa na
Comoro huko nilifanya shoo kubwa sana ambazo siwezi
kuzisahau.
Mwanaspoti: Ni shoo ipi iliyowahi kukuingizia pesa kubwa
kuliko zote?
Diamond: Shoo ile ya Mlimani City ya Diamond Forever, ile
iliniingizia pesa kubwa sana na tangu pale ndipo
nilipoanza kufurahia matunda ya kazi yangu. Nilifanya
shoo pia Burundi, Mombasa na Congo shoo hizi
ziliniingizia kiasi kikubwa sana cha pesa siwezi kutaja ni
shilingi ngapi lakini ni pesa nyingi ambazo sitakaa
nizisahau.
Mwanaspoti: Shoo ipi ilikuwa ya bei chee ambayo huwezi
kuisahau
Diamond: Kwa kweli siwezi kusahau nilipofanya shoo
yangu ya kwanza kubwa mwaka 2009 kwenye Fiesta
iliyofanyika Dar es Salaam, ilikuwa ndiyo shoo yangu ya
kwanza na kubwa wakati huo nilikuwa natamba na wimbo
Kamwambie, ilinichukua muda mrefu sana kujiandaa mimi
pamoja na madansa wangu wanne tulilipwa Sh 50,000
lakini sikukata tamaa kwani ilikuwa ndiyo mwanzo wangu
wa kujuana na watu wengi na wadau wakubwa wa muziki
hapa nchini ambao nilikutana nao kwenye ile shoo.
Mwanaspoti: Kwa hivi sasa ni shoo gani ambayo unaweza
kusema kwamba utafanya kwa bei ya chini na ni shilingi
ngapi?
Diamond: Shoo ninayoweza kufanya kwa bei ya chini
kabisa ni Sh 10 milioni za Kitanzania na hii labda nione
anayeniomba nifanye shoo hiyo hayuko vizuri na pengine
ni rafiki yangu na hawezi kuninyonya, si hivyo tu
itategemea pia ni kampuni gani na ni watu wa aina gani
ambao watanitaka nifanye nao kazi.
Mwanaspoti: Kwa kawaida Diamond ni msanii wa gharama
gani kwa shoo moja ndani na nje ya nchi?
Diamond: Kwa kawaida shoo moja ninafanya kuanzia Sh15
milioni mpaka Sh20 milioni kulingana na muda
nitakaofanya shoo. Pia zile za nje ninafanya kwa gharama
ya Dola 20,000 mpaka 30,000 yaani ni Sh32 milioni mpaka
48 milioni hivi kwa fedha za Tanzania na nikiwa huko
nahakikisha ninafanya kazi vile inavyotakiwa. Lakini hali ni
tofauti inavyokuja shoo ile ya uwanjani yaani hapa
nazungumzia shoo kubwa zinazofanyika nje ya ukumbi,
hizi natoza Dola 20,000 ambayo ni sawa na Sh32 milioni
32 kwa fedha ya Kitanzania.
Mwanaspoti: Kuhusu madansa wako unawachukuliaje?
Diamond: Ni kama kaka zangu na ninawapenda sana kwani
tumetoka nao mbali na wanajua kuwa tunafanya kazi
pamoja kutengeneza maisha hivyo ni kama ndugu zangu
na tunasaidiana kwenye kila jambo ukizingatia kuwa kile
tunachokipata tunagawana. Kwa kweli najitahidi sana
kuwaambia hasa kuhusiana na masuala ya kimaisha,
nahusika katika maisha yao ya kila siku na nijuavyo mimi
nikikosea tu mmoja akapotea kundi langu litakuwa
limeharibikiwa maana kila mtu namtegemea kwa upande
wake. Kwa sasa wamejenga nyumba zao na wanaendelea
vizuri kimaisha hilo ndilo sharti langu lazima wafanye
mambo ya maendeleo kwa kile tunachokipata.
Mwanaspoti: Umesafiri nao nchi ngapi, na kwanini
unapenda kuambatana nao?
Diamond: Nimesafiri nao sehemu mbalimbali kama Burundi,
Comorro na sehemu nyinginezo ambako nimekwenda
kufanya shoo, sina tabia ya kusafiri peke yangu hata
nikienda Ulaya na hata Marekani lazima niwe nao.
Ninapenda kuwa nao kwani ni sehemu ya muziki wangu na
imefika wakati nimekuwa nataka mapromota kuhakikisha
wanatulipia mimi na madansa wangu kwa ajili ya shoo
hasa tutakapojua kuwa shoo fulani itaingiza watu wengi au
udhamini mkubwa.
Mwanaspoti: Kuna safari ambayo umewahi kusafiri peke
yako?
Diamond: Ziko nyingi, nilienda mwenyewe kutokana na
ukubwa wa shoo, lakini ni miaka kadhaa nyuma, baadaye
nilijiwekea mikakati kwamba siwezi kusafiri mwenyewe
wakati shoo nahitaji kufanya na madansa wangu, awali
mapromota walikuwa wagumu kunielewa na wapo
waliokataa. Niliachana nao na kuwataka wakishajipanga
na kuhakikisha kwamba wanaweza kunichukua mimi na
madansa wangu watafanya hivyo.
Mwanaspoti: Umewahi kuwatema madansa?
Diamond: Sijawahi kubadilisha madansa kwa sababu
wanajua kazi yao. Ingawa nilikuwa na madansa sita
nilipokuwa naanza muziki lakini niliachana na wawili
kutokana na utendaji wao wa kazi. Wawili hawa hawakuwa
wabunifu kila siku walikuwa na staili ileile, niliamua
kuchagua vichwa ambavyo vikikaa na mimi mwishowe
tunatoka na kitu makini na chenye kueleweka. Kulikuwa na
tatizo pia la kukosea stepu wakati wa shoo hili lilikuwa
likinishushia sana hadhi yangu jukwaani, hapo ndipo
nilipoamua kuwaondoa.
Mwanaspoti: Kwa upande wa malipo unawalipaje?
Diamond: Ninawalipa vizuri lakini siwezi kutaja kiwango ila
ingekuwa kwangu ningetaja, hiyo ni haki yao wao wenyewe
kutamka ila mimi siwezi kutaja. Malipo ninayowalipa yapo
machoni mwa watu wanaowazunguka, dansa kujenga
nyumba kumiliki baadhi ya biashara si jambo dogo, hivyo
ninawalipa vizuri. Na hata gharama za kusafiri ndani na nje
ya nchi vyote ni juu yangu, malipo tunayoyapata
tunagawana.
Mwanaspoti: Unakumbana na changamoto zipi katika kazi
yako?
Diamond: Nakumbana na mengi, kwanza unapokuwa
msanii unayeongoza lazima upate vikwazo vingi.
Nakumbana na watu wengi wanaonichukia na kunitusi bila
sababu za msingi, hata hivyo nasingiziwa vitu vingi
ambavyo havipo nadhani hii ni changamoto iliyotokana na
kufanya vizuri katika muziki.
Wapo ambao wanamwona Diamond anafanya vizuri
kwenye muziki badala ya kukaa na kuangalia nimepita
wapi na wapi anaanza kutoa lawama kwamba ameibiwa na
mengine ambayo kimsingi hayana maana.
Mwanaspoti: Siku za hivi karibuni kuna maprodyuza na
wasanii wasiofahamika ambao walijaribu kutengeneza kazi
yako ya My Number One na kukutusi kupitia wimbo huo na
wapo waliotunga mashairi mengine yaliyozungumzia
maisha yako kabla hujawa staa, ulijisikiaje? Na unachukua
hatua gani?
Diamond: Awali niliumia sana nilipoibiwa mashairi ya
wimbo wangu wa Mbagala, iliniuma sana kwa muda wa
wiki nzima uchungu nilioupata siwezi kuuelezea. Lakini
baadaye nilikomaa, huwezi amini niliposikia zile nyimbo
nilicheka sana kisha nikawadharau sana watu waliofanya
hivyo maana nipo kwenye hii tasnia siwezi kuchukia watu
wasiojua walitendalo kwani na wao wapo katika kujitafutia
riziki. Lakini hata hivyo sheria ya muziki bado haijawa
makini hapa nchini
nitachukua hatua gani mwisho wa siku nitaacha kufanya
mambo yangu ya msingi na kushughulikia wezi wa kazi
zangu ambao hata hivyo hawatabanwa kwa lile
walilolifanya.
Mwanaspoti: Msanii yupi hapa Tanzania anakutisha kama
hayupo vipi huko nje ya nchi?
Diamond: Kwa hapa Tanzania sijaona mwanamuziki
anayenitisha, ila siwezi kujua mashabiki wao ndio majaji,
nafikiri kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake. Kati ya
wanamuziki ninaowahusudu mimi kwa nje ya nchi hasa
Afrika ni P Square pekee, hawa wapo katika nafasi kubwa
sana kwenye ubongo wangu na nafikiria ni lini ninaweza
kuwafikia, hiyo ndiyo ndoto yangu daima.
Mwanaspoti: Unapokuwa juu ya jukwaa unakumbana na
vishawishi vipi ukiwa kama msanii mkubwa?
Diamond: Ninapata vishawishi vingi sana ninapokuwa
jukwaani. Kwa kweli ninashawishiwa na wakinadada,
mfano kuna mwanamke mmoja ambaye alikuwa mmoja wa
mapromota wa shoo nchini Uingereza alitaka kunibusu
mdomoni kwa lazima, kitendo kile kilinifedhehesha sana na
nilishindwa nifanyeje kwani nipo ugenini na jukwaani
ilikuwa ngumu sana kwangu. Wakati mwingine wanawake
wanapanda jukwaani ili wacheze na wewe mwisho wa siku
wanaingiza mikono kwenye suruali yaani sipendezwi
kabisa na michezo ya namna hii.
Mwanaspoti: Umewahi kuibiwa ukiwa jukwaani?
Diamond: Nimeshaibiwa sana hasa katika hizi shoo ndogo
ndogo mara nyingi watu wanapanda jukwaani na kuondoka
na kitu chako. Nakumbuka nimeshawahi kuibiwa saa, pete
ya dhahabu na kuna mmoja alitoa kali ya mwaka yaani
yeye alinivua nguo kwa lazima.
Mwanaspoti: Inakuwaje nje ya muziki, unakumbana na
changamoto zipi?
Diamond: Kitu ambacho ni changamoto kubwa sana
kwangu ni simu yangu ya mkononi. Kila baada ya miezi
sita au mitatu nalazimika kubadili namba yangu ya simu,
nasumbuliwa sana na watu ambao hata hivyo hawana la
msingi la kuniambia. Ni kweli kwamba mawasiliano ni kitu
cha msingi na
ninawapenda mashabiki wangu lakini namba yangu
inasambaa kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba nashindwa
kupokea simu za maana kwa kudhani kwamba na hao nao
ni wasumbufu.
Mwanaspoti: Ina maana milio yote ya simu hapo ni watu
wanakupigia?
Diamond: Yap, unavyoona inalia kila dakika watu wanapiga
hapa. Muda mwingi hii simu ninaweka 'silent' yaani haitoi
mlio wowote kwani inaita kila dakika.
Mwanaspoti: Tuzungumzie uhusiano wako. Mpenzi wako
wa kwanza unamkumbuka? na je uliwahi kumpa shilingi
ngapi?
Diamond: Mpenzi wangu wa kwanza kabisa enzi hizo
ninajifunza mambo haya sikumbuki vyema jina ila alikuwa
anaishi Tandale na mimi pia nilikuwa naishi huko na mama
yangu. Sikumbuki kama nimewahi kumhonga maana enzi
hizo mimi nilikuwa napewa tu na mama yangu pesa,
sikuwa na hela yoyote ya kumpa na ilikuwa ni kwa kipindi
kifupi kama miezi minne hivi, hata hivyo tulikuwa
tunaibana tu kwa siri nilikuwa mdogo.
Mwanaspoti: Kwanini mliachana?
Diamond: Kwanza nilikuwa sijajua mapenzi ni nini. Hata
hivyo haikuwa rasmi na wala nilikuwa sijawa na akili ya
kupenda sana na nilikuwa na fikra kwamba ni mchezo tu
hivyo tuliachana mapema kwani hata yeye akili yake
ilikuwa haijakomaa.
Mwanaspoti: Mpenzi wako uliyekuwa naye kabla ya kuwa
staa nasikia uliachana naye baada ya kutoka kimuziki kwa
nini?
Diamond: Nilimpenda sana lakini aliniacha kabla ya
kutoka. Mpenzi wangu wa kwanza alikuwa anaitwa Sarah
Sadick, sijawahi kumuhonga na ndiye mwanamke
niliyewahi kumpenda sana. Wakati huo Naseeb Abdul kabla
sijawa Diamond nilikuwa nahaha kuhangaika ni vipi
nitatoka kimuziki. Msichana huyu ndiye aliyenipa hasira za
kufanya muziki kwa bidii zote baada ya kunitema na
kuanza kuhangaika na wengine na aliniita majina mengi
yasiyo mazuri, kisa sina fedha. Si kwamba nilimuacha bali
yeye ndiye aliyeniacha kama zali baada ya wiki kadhaa
nikatoka na wimbo Kamwambie, taratibu nikaanza kuwa
staa naye akaanza kurudi ila nilishamuondoa moyoni
mwangu.
Mwanaspoti: Kwa nini mliachana? Unadhani hakukufaa
tena kwa kuwa ulishakuwa staa?
Diamond: Alinisumbua sana kutokana na ugumu wa
maisha niliokua nao kwa kipindi cha nyuma hadi kufikia
2009. Nilimpenda sana huwezi amini nilikuwa silali
usingizi kwa ajili yake. Nahisi ilitokana na mimi kukosa
kazi ndiyo maana ilifikia hatua alinipotezea. Lakini baada
ya kupata na kujulikana alinifuata lakini sikutaka tena hata
baada ya kuniomba msamaha.
Mwanaspoti: Umewahi kuwa na wanawake wangapi tangu
uwe staa?
Diamond: Sikumbuki kwa kweli wapo wengi mno, si unajua
tena wapo walionitaka na kunilazimisha nifanye hivyo,
lakini idadi kamili siwezi kukumbuka na kila siku
nasumbuliwa na hawa wanawake.
Mwanaspoti: Ni wapenzi wangapi ambao umekuwa nao
kipindi kirefu na kuwapenda kama wapenzi wako?
Diamond: Nimewahi kuwa na wapenzi wanne katika kipindi
chote cha ustaa wangu na sikupenda kubadili ovyo ila
wengi wao hawakuweza kutimiza haja ya moyo wangu.
Mwanaspoti: Unaweza kuwataja majina?
Diamond: Ndiyo ila wawili wanafahamika zaidi. Wa kwanza
kabisa alikuwa anaitwa Sarah na wa pili alikuwa anaitwa
Hawa yule msichana niliyeimba naye katika wimbo
'Nitarejea', huyu alizidiwa ujanja na Wema Sepetu ambaye
naye alikuja kuondoka kwangu na baadaye nikawa na
Penieli Mungilwa.
Mwanaspoti: Mwanamke yupi unahisi ulimpenda kuliko
wote?
Diamond: Mwanamke wangu wa kwanza Sarah Sadick
huyu aliniingia sana moyoni sijajua ni kwanini. Lakini
nahisi huenda kwa kuwa awali alinipenda kweli kwa kuwa
wakati huo sikuwa na kitu. Hata hivyo nahisi ilitokana na
mimi kutokuwa bize na wakati huo sikufikiria lolote zaidi ya
yeye ilitokana na kutokuwa na kazi ya kufanya. Siku hizi
sina mapenzi ya kivilee, nawaza zaidi pesa na
ninaihangaikia na zaidi ni muziki wangu, hili ndilo la
kwanza kabisa linalonifanya niwe bize mapenzi baadaye.
Mwanaspoti: Umeshawahi kutongozwa na wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna mmoja kati ya
wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye
mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika
uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza kumfikiria
mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi
mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa
sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp,
Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao
wanatafuta namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Unapata usumbufu wowote toka kwa
wanawake?
Diamond: Ndiyo, wengi sana tena kuna mmoja kati ya
wanawake niliowahi kuwa nao alinitongoza yeye
mwenyewe ndipo nikawa naye na nilikaa naye katika
uhusiano kwa kipindi kirefu tu. Wanaweza kumfikiria
mwanamke fulani lakini huwezi amini ukweli ninao mimi
mwenyewe na katu hawawezi hata kumhisi. Ninatongozwa
sana kwenye mitandao ya kijamii, facebook, whatsapp,
Instagram na kwingineko na wapo wasichana ambao
wanatafuta namba zangu za simu na kuanza kunisumbua.
Mwanaspoti: Ni mwanamke wa aina gani unataka awe
mkeo?
Diamond: Kwanza ninahitaji aijue kazi yangu na ajue
kwamba mimi ni mtu maarufu hivyo akubaliane na
changamoto mbalimbali atakazokumbana nazo kwa kipindi
atakachokuwa ndani ya ndoa, siyo siku mbili anafungasha
virago. Pia ajue kwamba nitamsikiliza mama yangu
kwanza kabla ya yeye hilo naliweka wazi, yeye ana nafasi
yake katika maisha yangu lakini mama yangu nimempa
kipaumbele, tatu awe tayari kuishi na mama yangu. Nne
awe na akili na mwenye utambuzi na atakayeniongoza
katika kazi zangu, sihitaji. Itaendelea…
Chanzo: mwanaspoti

No comments:

Post a Comment