Thursday, 28 November 2013

BAADA YA ZITTO KUVULIWA UONGOZI VIJANA CHADEMA WACHAPANA MAKONDE NA KUCHANA BENDERA MKOANI MBEYA


Uamuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) wa kuwavua nafasi za uongozi vigogo
wake watatu akiwamo aliyekuwa Naibu Katibu
Mkuu, Zitto Kabwe, umepokelewa vibaya na baadhi
ya wafuasi wao ambao wameamua kupigana
ngumi na kuchana bendera za chama hicho.
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
alivuliwa nyadhifa zake sambamba na aliyekuwa
mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Mkumbo Kitila na
aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa
Arusha, Samson Mwigamba.
Kamati Kuu ya chama hicho ilichukua hatua hiyo
Ijumaa iliyopita, baada ya kubaini waraka wa
usaliti waliouandaa ukiibua tuhuma mbalimbali
dhidi ya chama na viongozi wake ngazi ya taifa.
NGUMI ZAPIGWA MBEYA
Kundi la vijana wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa
Zitto jijini Mbeya wanadaiwa kuchana bendera za
chama hicho na kurushiana makonde na viongozi
wa Chadema katika ofisi ya chama hicho Wilaya ya
Mbeya Mjini kwa madai ya kutofautiana msimamo
kuhusiana na uamuzi wa Kamati Kuu.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini,
David Mwambigija maarufu kwa jina la ‘Mzee wa
Upako’, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo juzi
mchana.
Mwambigija alisema kuwa chanzo cha vurugu hizo
ni vijana zaidi ya 18 wanaodaiwa kuwa ni wafuasi
wa Zitto kuanza kufanya vikao vya siri mjini
Mbeya kwa nia ya kukihujumu chama.
Alisema uongozi wa chama ngazi ya wilaya
ulipopata taarifa hizo alizodai kuwa ni za
kiintelijensia na kuwa yeye (Mwambigija) ambaye
ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya chama hicho
wilaya, aliamua kuwaandikia barua ya kuwaita
ofisini kwa lengo la kuwahoji.
Alisema vijana hao walipofika ofisini kwake huku
wajumbe wa Kamati Tendaji wakiwa tayari
wameketi kwa ajili ya kuwahoji, waliingia ndani ya
ofisi na kulazimisha wahojiwe kwa pamoja badala
ya kuhojiwa mmoja mmoja.
Alisema walipotakiwa watoke nje ili kila mmoja
ahojiwe kwa wakati wake, waligoma na kukataa
kutoka ofisini na ndipo yeye kama Mwenyekiti
alipoamuru kikosi cha ulinzi wa chama hicho
maarufu kwa jina la Red Bridged kuwatoa nje kwa
nguvu na ndipo vurugu hizo zilipoanza.
“Ni kweli kumetokea vurugu kubwa ofisini kwetu
wakati kikao cha kamati ya utendaji kikihitaji
kuwahoji vijana wanaoendesha vikao vya siri
kutaka kukihujumu chama kutokana na uamuzi wa
Kamati Kuu kumvua Zitto madaraka, tumepata
taarifa hizi kwa njia zetu za kiintelijensia kuwa
vijana hawa wapo kwenye kundi la Zitto,” alisema
Mwambigija.
Hata hivyo, Mwambigija alipotakiwa kuonyesha
uthibitisho juu ya tuhuma dhidi ya vijana hao,
alisema kuwa ushahidi bado ni siri kwa vile
wametumia njia zao za kiintelijensia kubaini
mtandao wa vijana hao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana
Mkoa wa Mbeya, Joseph Kasambala ambaye ni
mmoja wa vijana walioitwa kuhojiwa na kamati ya
utendaji alikanusha madai hayo na kusema kuwa
vurugu hizo hazikuwa na uhusiano hata kidogo na
usaliti wa chama.
Alisema chanzo cha vurugu hizo ni Kamati hiyo
kumuita na kutaka kumuhoji kinyume cha katiba
ya Chadema yeye (Kasambala) ambaye ni kiongozi
wa mkoa, hivyo hawezi kuhojiwa wala
kuwajibishwa na kamati hiyo ambayo ni ngazi ya
wilaya.
Alisema kuwa Katiba ya Chadema inaeleza wazi
kuwa kingozi wa mkoa mamlaka yake ya nidhamu
ni Kamati Kuu ya Chadema Taifa, hivyo kitendo
cha ngazi ya wilaya kumuita na kutaka kumuhoji ni
ukiukwaji wa Katiba.
“Mimi baada ya kupata barua ya kuitwa na
Kamati hiyo ikinieleza kuwa nina tuhuma ambazo
hazikuandikwa kwenye barua waliyoniletea,
nilikwenda ofisini ili nipewe tuhuma zangu kwa
maandishi kama ambavyo Katiba inaelekeza, lakini
nikashangaa eti wanataka wanihoji, nikakataa
walipotaka kunishinikiza vijana wakawajia juu
wakipinga nisidhalilishwe na ndipo vurugu zile
zilipoanza,” alisema Kasambala.

No comments:

Post a Comment