Dar/Kigoma. Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutangaza kumvua uanachama, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kesho atatua jimboni kwake kuzungumza na wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Uamuzi
wa kumfukuza Zitto (pichani) ulifikiwa juzi ikiwa ni muda mfupi baada
ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi aliyofungua Januari 2, 2014, dhidi
ya Bodi ya Wadhamini na katibu mkuu wa Chadema, iliyokuwa imeshikilia
uanachama wake.
Mwanasheria
mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ndiye alitangaza kutimuliwa kwa Zitto
akisema ni kutokana na kufungua kesi mahakamani, kinyume na Katiba ya
Chadema kipengele cha 8 (a) (x).
Jana,
Zitto ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) aliongoza kikao cha kamati hiyo, kilichojadili taarifa ya Tanesco
na baadaye alisisitiza kwamba hana taarifa rasmi ya uamuzi wa mahakama
na atakapoipata atazungumzia hatima yake.
“Kama
mnavyoona mimi naendelea na kazi na wala sina taarifa rasmi lakini
nikipata taarifa rasmi na mimi nitatoa taarifa rasmi, Ijumaa (kesho)
ninakwenda jimboni kuzungumza na wapigakura wangu ambao niliwaahidi
kufanya hivyo kabla ya vikao vya Bunge kuanza Jumanne ijayo,” alisema
Zitto ambaye taarifa zinasema alikuwa amepapanga kuwaaga wapiga kura na
baadaye kutimkia kwenye chama kipya cha ACT alichokiasisi.
“Muhimu
kwangu ni kufanya kazi ya Watanzania na nitafanya kwa mazingira yoyote
yale. Siasa yangu inajikita katika masuala, siyo watu, ukiandika kuhusu
Zitto siyo kwa ajili ya mtu bali masilahi ya Taifa.
“Nakuzwa, nakomazwa na hii ni changamoto, nitaendelea kufanya kazi zangu hadi nitakapopata taarifa rasmi.”
Mwanasheria
wa Zitto, Albert Msando juzi aliliambia paparazi kwamba, anafuatilia
uamuzi huo wa mahakama kabla ya kuona ni hatua gani watazichukua.
Baadhi
ya wanachama na viongozi wa Chama cha ACT mkoani Kigoma wamedai
kufurahishwa na uamuzi huo, wakidai kuwa utakinufaisha chama hicho.
Mkazi
wa Mwandiga, Dunia Pemba alisema Zitto alipaswa kujiondoa ndani ya
Chadema pale tu alipovuliwa nyadhifa zake ili atazame sehemu nyingine
yenye demokrasia pana kwa vile chama hicho kilionyesha hakimhitaji tena.
“Sisi
tulitangulia huku ACT na sasa tunamsubiri kwa hamu, aje kujenga chama
hiki ambacho ni tishio kubwa hapa nchini na bila shaka kitachukua viti
vingi vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ndiyo maana
kutimuliwa kwa Zitto Kabwe ni faraja kwetu kwa sababu atapata muda wa
kutosha kujenga chama,” alisema Pemba.
Pia,
mwenyekiti wa vijana wa ACT Tawi la Mwandiga, Stili Chuma alisema
anafurahia uamuzi ya Chadema ingawa kitendo cha jimbo lake kukosa
mwakilishi kinasikitisha.
Katibu
Mwenezi wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini, Shaban Kasugulu
alipongeza uamuzi wa Mahakama Kuu akidai haki imetendeka kwa vile suala
la Zitto na Chadema lilichukua muda mrefu na kusababisha watu kukosa
mwelekeo.
Hata
hivyo, Boaz Chuma aliitupia lawama Mahakama Kuu kwa kuibeba Chadema
katika shtaka hilo kutokana na kutoa hukumu siku ambayo haikupangwa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema
kufutwa uanachama kwa Zitto ni fundisho kwa wananchi ambao licha ya
kuchagua mbunge wanayempenda, lakini anaweza kuondolewa na vyama vyao.
“Wananchi
wanamchagua mbunge wao kupitia chama cha siasa lakini hawawezi
kumwajibisha hadi baada ya miaka mitano,” alisema na kuongeza kuwa ni
chama pekee kinachoweza kumwajibisha.
Dk
Makulilo alisema katika rasimu ya Katiba iliyokuwa ikipendekezwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulikuwa na kipengele kilichotaka wananchi
wawe na uwezo wa kuwajibisha wabunge wao, lakini kikaondolewa na Bunge
Maalumu la Katiba.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk Emmanuel Mallya kuondolewa kwa Zitto ni
taratibu na kanuni za chama kilichompitisha kugombea nafasi hiyo na hapo
ndipo unaona umuhimu wa kuwapo mgombea binafsi ili wananchi wawe na
nguvu zaidi,” alisema Mallya.
Mbunge wa Mbarali, Modesti Kilufi alisema bado wanaamini Zitto ni mbunge, bado ni mwenyekiti wangu na anaweza kukata rufaa.

No comments:
Post a Comment