.jpg)
Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaachia huru Mwenyekiti wa
Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum
Development Corporation – TPDC) Mh. MICHAEL PETRO MWANDA na Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo JAMES ANDILILE kusubiri ufafanuzi wa
Bunge kutokana na tuhuma zinazowakabili. Awali, jana tarehe 03/10/2014
saa tano asubuhi katika ukumbi wa Bunge uliopo jijini Dar es Salaam
katika chumba cha mikutano kulikuwa na kikao cha Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali, Mwenyekiti akiwa ni Mh. ZITTO ZUBERY KABWE (MB) na
makamu wake ni Mh. DEO FILIKUNJOMBE (MB).
Katika
kikao hicho agenda ya mkutano ilikuwa ni kuwasilisha mahesabu ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kipindi
kinachoishia tarehe 30 June, 2013. Baada ya majadiliano ya muda kuhusu
hati mbalimbali zilizotakiwa na Kamati hiyo ya Bunge hatimaye Mwenyekiti
wa Kamati Mh. Zitto Zubery Kabwe alitoa maagizo kwa askari wa Polisi
waliokuwepo katika eneo hilo kwa masuala ya ulinzi kuwa Mwenyekiti wa
bodi ya TPDC na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wafikishwe kituo cha polisi Kati.
Kutokana
na maelezo ya mashahidi waliokuwepo kwenye tukio hilo katika ukumbi wa
Bunge Mwenyekiti Zitto alisema wapelekwe Polisi waende kusubiri mwongozo
wa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye
atawasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa maagizo ya mwisho. Mara
baada ya agizo hilo watu hao walifikishwa kituo cha Polisi Kati chini
ya ulinzi.
Uongozi
wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ulishindwa kuchukua
hatua zaidi ya hapo kwani shauri hilo halikuwa na mlalamikaji aliyekuja
kufungua jalada na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili
viongozi wa TPDC. Aidha, maafisa wawili wa secretarieti ya Bunge
waliitwa Polisi kutoa ufafanuzi kuhusu kadhia hii wakiwepo pia mawakili
wa watuhumiwa na hatimaye kilifanyika kikao cha dharura ili kupata
ufafanuzi wa kisheria.
Hatimaye
iligundulika kwamba katika sheria ya HAKI, KINGA na MADARAKA ya Bunge
sura ya 296 Kif 12 (3) kinaonyesha kwamba mwenyekiti wa Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali alitakiwa kwanza apendekeze kwa Mhe. Spika wa
Bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa.
Mhe.
Spika akisharidhika kuhusu tuhuma zozote zilizoletwa mezani kwake na
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, ndipo anamwandikia Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa ni pamoja na
hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa.
Katika
kikao hicho na jopo la wanasheria iligundulika kwamba katika sheria ya
Haki, Kinga na Madaraka ya bunge, agizo la kukamatwa watu hao
lililotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge lilihita kuzingatiwa kwa
taratibu tajwa hapo juu kwanza kabla ya utekelezaji wake.
Hatimaye
ilionekana hakuna sababu ya kuendelea kuwashikilia viongozi hao na
badala yake wameachiwa huru tukisubiri taratibu na sheria kama
ilivyoelezwa hapo juu.
S.H. KOVA
No comments:
Post a Comment