Ndugu
viongozi wote wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi diaspora, wawakilishi
wa serikali ya Tanzania ndani na nje ya nchi, taasisi za kitaifa na
kimataifa, mashirika ya kijamii, mashirika binafsi, viongozi mbalimbali;
itifaki imezingatiwa.
Awali
ya yote napenda kumshukuru M/Mungu kwa kutupa uzima na afya njema
kuweza kutekeleza majukumu yetu ya kila siku ikiwemo kusimamia sera na
utendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama
Cha Mapinduzi huku diaspora. Pia napenda kuchukua fursa hii kumshukuru
na kumpongeza Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na M/kiti wa
Chama Cha Mapinduzi kwa kuchagua mwakilishi wa Diaspora kutuwakilisha
kwenye mchakato huu na kuona umuhimu wa kufungua matawi ya CCM nje ya
nchi. Ni wazi raisi wetu anatujali, anatupenda na kututhamini na sisi
tunamuahidi kumuunga mkono ktk kila nyanja ya maendeleo.
Nikiwa
kama mratibu wa matawi ya Chama Cha Mapinduzi Marekani na Muwakilishi
wa Matawi ya Diaspora; mimi Loveness Mamuya kwa niaba ya wana CCM wote
waishio Marekani na Diaspora tunapenda kutoa pongezi za dhati kwa Dr
Jakaya Mrisho Kikwete (Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania) pamoja
na Dr Ali Mohamed Shein (Raisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) kwa
kuanzisha, kusimamia na kufanikisha mchakato wa katiba mpya na hatimaye
kupatikana kwa katiba inayopendekezwa. Ni wazi kwamba hekima, busara,
weledi na upendo wenu kwa Tanzania ni hazina isiyo futika. Sisi wana CCM
diaspora tumefarijika sana na tunathamini jitihada zenu za ziada ktk
kupambana na changamoto mbalimbali ambazo zilikuwa na malengo ya
kukwamisha mchakato huu. Aidha tunawaombea maisha marefu yenye utulivu
na mafanikio kwa kipindi chote hiki hadi kuelekea 2015 mkapate kutimiza
ahadi ya kuvikamilisha vipengele muhimu vya katiba inayopendekezwa.
Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche
majina yenu kwa wino wa dhahabu.
Shukrani pia zimuendee Mh
Samuel Sitta (M/kiti wa Bunge Maalum la Katiba) pamoja na makamu wake Mh
Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia kanuni, sheria na taratibu
zilizowekwa na hatimaye kufanikisha zoezi zima la kupatikana katiba
inayopendekezwa. Ni wazi kwamba kazi yenu haikuwa rahisi na kuna kipindi
iliwabidi mfanye maamuzi magumu lakini kasi na viwango vyenu
vimetupatia katiba inayopendekezwa mapema kabla ya kikomo mlichowekewa.
Ari na kujitoa kwenu kusimamia bunge la katiba ni historia ambayo
itasomwa na vizazi vyote vya watanzania. Nyinyi ni mashupavu na mashujaa
wa vita dhidi ya matabaka yote ya vyama vya siasa, udini na ukabila na
hatimaye mmefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kutupatia katiba ambayo
inawajali watanzania wote licha ya tofauti zetu za kimazingira,
kiutawala na kiufanisi. Mapenzi yenu ya dhati kwa Tanzania yetu ni
ishara ya matumaini na imani ya Tanzania njema huko mbeleni. Kama taifa
linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu
kwa wino wa dhahabu.
Shukrani za dhati ziwafikie
wajumbe wote wa bunge maalum la katiba kwa kuchambua, kuboresha na
kurekebisha mambo ya msingi yanayohusu taifa letu pamoja na kutanguliza
maslahi ya taifa kwanza. Umakini na uwajibikaji wenu ndio silaha ya kila
mtanzania ktk kuifikia dira ya maendeleo ya taifa letu. Asanteni kwa
kutambua makundi yote ktk jamii na kuyatendea haki. Asanteni kwa kuwa
mabalozi wa wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimba madini, wafanya
biashara wakubwa na wadogo, sekta binafsi, walemavu, wakina mama,
wasomi, vijana, watoto na wazee. Hii imetudhirishia kwamba uteuzi wa Dr
Jakaya Mrisho Kikwete kwenu ni wa busara na wa kipekee. Hongereni sana
kwa kazi nzuri mliyoifanya na tunaamini hata yule mjumbe aliyetangulia
mbele ya haki anajivunia kazi nzuri mliyoifanya. Mungu aendelee kuilaza
roho yake mahala pema peponi. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti
ya nchi yetu, basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila na
shukrani kama sitatoa pongezi zangu za dhati kwa tume ya mabadiliko ya
katiba chini ya M/kiti wao Mh Joseph Sinde Warioba kwa kutupatia rasimu
ya katiba mpya ambayo ndio msingi wa kwanza na wa muhimu ktk upatikanaji
wa katiba mpya. Katiba inayopendekezwa ina 82% ya michango yenu na
hivyo ni wazi kwamba mnastahili pongezi kwa juhudi na uadilifu wenu ktk
kukusanya, kuchambua na kuwasilisha rasimu ya katiba. Hakika watanzania
tunajivunia umahiri wenu na tutawakumbuka ktk kila hatua ya mendeleo ya
taifa letu. Kama taifa linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu,
basi yakafiche majina yenu kwa wino wa dhahabu.
Mwisho kabisa, natoa ari kwa
watanzania hasa wana CCM wote ndani na nje ya nchi kwamba safari bado
inaendelea, kupata jambo lolote zuri ni lazima tupambane. Tunawaomba
watanzania wote tukapambane ktk zoezi la kupiga kura kwa kuiunga mkono
katiba inayopendekezwa. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuisoma, kuipitia
na kuielewa katiba inayopendekezwa na kuwaelimisha wale ambao hawawezi
kufanya uchambuzi wa kina. Hayati Mwl Nyerere alisema watanzania tuna
maadui watatu; nao ni umaskini, ujinga na magonjwa. Leo hii wapo
matajiri wa uwezo lkn maskini wa mawazo, wapo wasomi wa vyeti lkn
wajinga wa kufikiri na wapo wazima wa afya lakini wagonjwa wa akili.
Hawa ndio maadui zetu watanzania, twendeni tukapambane nao na tusikubali
watuyumbishe kwa namna yoyote ile. Tukaipigie katiba inayopendekezwa
kura ya NDIO ili tupate katiba ambayo itatuvusha mbele kwa zaidi ya
miaka 50 inayokuja. Mungu akatubariki na akatuongoze ktk kusimamia,
kuitetea na kuipigania Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama taifa
linavyoweza kuficha mambo nyeti ya nchi yetu, basi yakafiche majina ya
watanzania wote watakao ipigia katiba inayopendekezwa kura ya NDIO kwa
wino wa dhahabu.
Mwisho kabisa, naomba
watanzania wenzetu mtambue kwamba nchi yetu inasifika duniani kwa
amani, umoja, utulivu na upendo. Kuna jitihada za makusudi zinafanywa na
baadhi ya watu wasio na malengo ya dhati na nchi yetu kuweza kuichafua.
Kwa pamoja tuwatambue, tusikubali na tujiweke mbali na watu hawa. Kwa
pamoja tukaijenge Tanzania bora ya vizazi vyetu vya jana, vya leo na vya
kesho. Waswahili wanasema, "mkataa kwao ni mtumwa." Sisi wana CCM
diaspora tunaipenda na tutaendelea kuiwakilisha Tanzania yetu popote
tuendako. Hongera Dr Jakaya Kikwete, Hongera Dr Ali Mohamed Shein!
Shime Chama Cha Mapinduzi. Mungu ibariki Tanzania, Mungu wabariki
watanzania.
Asanteni sana.
Imewasilishwa na Ndugu Loveness Mamuya;
Kada Mzalendo na Mratibu wa Matawi ya Chama Cha Mapinduzi,
(USA/ Diaspora)
No comments:
Post a Comment