WAFANYABIASHARA wa maduka ya soko la Kariakoo wameanza mgomo kwa muda usiojulikana kuanzia jana, sambamba na kuishinikiza Serikali kupunguza kodi ya asilimia 18 wanayotozwa kupitia mashine za kielektroniki (EFDs).
Wamefikia hatua hiyo ikiwa ni siku moja baada ya TRA kutangaza
kufanya ukaguzi endelevu na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wale
watakaokaidi kutumia mashine hizo.
Wakizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam jana kwa nyakati
tofauti, wafanyabiashara hao walisema kuwa walifikia hatua ya kufunga
maduka ili kupinga makato ya kodi kubwa inayowakosesha maslahi.
Mmoja wa wamiliki wa duka la nguo, Kibatala Kimweli, alisema ameamua
kufunga duka ili asifanyiwe uhakiki na TRA, kwani tangu ameanza kutumia
mashine hizo amebaini kupata hasara inayotokana na kukatwa kodi ya
asilimia 18.
“Kilio chetu tunataka punguzo la kodi kwani ikiwa kubwa faida inakuwa
ndogo, ndiyo maana mnaona hali hii ya mgomo inaendelea, kama
walivyosema ni zoezi endelevu na sisi tutafunga maduka bila kuacha
halafu tuone watatoa wapi kodi na nani atatumia mashine zao,” alisema.
Kimweli alitaja sababu nyingine za kufunga maduka hayo kuwa ni
kutopatiwa elimu ya kutosha wafanyabiashara wengi, kama ilivyokuwa
imeamuliwa na Rais Jakaya Kikwete Aprili 22, mwaka huu.
Naye Halima Bakary, alidai kuwa mfumo unaotumiwa na Serikali
unawatoza kodi kubwa, hali inayowafanya wafanyabiashara wengi kukwepa na
kutumia njia nyingine zisizokubalika.
Akizungumzia kuhusu mgomo huo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa
Mlipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo, alisema
kwamba wao wataendelea kusimamia sheria kuhakikisha kila mfanyabiashara
anatumia mashine hizo kwa ajili ya kulipa kodi.
“Sheria tunazozitumia zimetungwa na wabunge ambao ndio
wanawawakilisha wafanyabiashara hao, hivyo suala la kusimamia sheria
lipo mikononi mwa TRA na hawatakuwa tayari kusimamisha uhakiki wa
mashine hizo kwa wafanyabiashara wadanganyifu na wale wasiozitumia
kabisa, lazima watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
Kayombo aliongeza kuwa wafanyabiashara hao wameanza mgomo baada ya
hivi karibuni kufanyika kwa ukaguzi wa kila duka na kubaini kuwapo kwa
baadhi yao wanaotumia mashine ambazo hazijasajiliwa TRA, ikiwamo na
wengine wasiozitumia.
Alisema kuwa wamebaini uwapo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiotoa
risiti halali kulingana na thamani ya bei ya bidhaa wanazouza.
Kayombo alisema TRA itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria
wafanyabiashara wanaoshawishi wenzao kufunga maduka na kuacha kutumia
mashine za EFD’s, kwani hadi sasa tayari baadhi yao wamekamatwa na
kufikishwa mahakamani.
Aliongeza kuwa katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam
maduka 70 yalibainika kutotumia stakabadhi, na kati yao 11 yamefungiwa.

No comments:
Post a Comment