WEZI WA NMB KUNYOGWA
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi, imetoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa
washitakiwa wawili raia wa Kenya, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya
mauaji ya askari polisi PC Michael Milanzi.
Washitakiwa hao walimua askari huyo katika tukio la uporaji wa fedha katika Benki ya NMB, tawi la Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mbali na hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu,
Kakusulo Sambo kwa zaidi ya saa nne, mshitakiwa wa tatu katika kesi
hiyo, Karisti Kanje (Mtanzania), amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka
mitano jela kwa kosa la kuhifadhi na kutorosha watuhumiwa wa mauaji ya
askari polisi.
Akisoma hoja zilizotolewa mahakamani hapo na pande za utetezi na ile ya
serikali, Jaji Sambo, alieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani
hapo na mashahidi 18 wa upande wa Jamhuri, mahakama iliridhika kuwa
haukuacha shaka yoyote kwa washitakiwa wote watatu.
Alisema kutokana na ushahidi wa shahidi wa 1, 3 na 11, mahakama
imeridhika kuwa washitakiwa wawili, Samwel Gitau Saitoti na mwenzake
Michael Kimani, raia wa Kenya, walimuua kwa makusudi PC Milanzi kwa
kumpiga risasi na kwamba inatoa adhabu kwa kila mmoja kunyongwa hadi
kufa.
“Mahakama imeridhika kwa namna ambavyo mashahidi namba 1, 3, 11
walivyoelezea ushiriki wa washitakiwa katika tukio hilo. Mahakama
imeridhika bila shaka yoyote kwamba washitakiwa hao walimuua kwa
kukusudia askari wetu, ambaye serikali bado ilikuwa ikimhitaji,” alisema
Jaji Sambo.
Alisema washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa na lengo moja la kutekeleza
ujambazi katika benki hiyo, waliamua kumuua PC Michael, kitendo ambacho
kisheria adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu 197
kanuni ya sheria namba 7.
Akieleza kwa kifupi maelezo ya shahidi namba 1, 3, na 11, ushahidi
unaotajwa kuwa muhimu uliowatia hatiani washtakiwa hao, Jaji Sambo,
alisema mashahidi wote walidai mahakamani hapo kuwa waliwaona wahusika
wa mauaji kwa karibu na hakuna ubishi kuwa ndio walihusika na mauaji
hayo.
“Shahidi namba tatu ambaye ni askari akiwa lindo na marehemu, aliieleza
mahakama kuwa mshitakiwa namba mbili (Kimani) alifika katika eneo la
benki na kuomba kuonana na mmoja wa wafanyakazi waliokuwa bado ndani ya
benki, ndipo marehemu akamuita mwenzake (shahidi namba 3) kwa
mashauriano ambayo hata hivyo wote walikataa ombi hilo.
“Baada ya muda, nyuma ya kibanda ghafla akatokea mshitakiwa namba moja
(Saitoti) akampiga kichwani PC Michael kwa kutumia kitako cha bunduki
ndipo yakazuka mapambano, mshitakiwa namba mbili akipambana na shahidi,
huku mshitakiwa namba moja akipambana na marehemu PC Michael,” alisema
Jaji Sambo kueleza maelezo ya shahidi namba tatu.
Alisema muda wote wa mapambano shahidi alikuwa akitazamana ana kwa ana
na washitakiwa, na kwamba baada ya kuzidiwa ndipo mshitakiwa namba mbili
akasikika akimwambia mwenzake (mshitakiwa namba moja) afyatue risasi
iliyompiga PC Michael na kuanguka chini.
Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo, wakili wa upande wa utetezi, Faustine
Materu, aliiomba mahakama ione kwamba miaka saba ambayo mshitakiwa namba
tatu, Karisti Kanje aliyokaa gerezani, inatosha kuwa adhabu yake ombi
ambalo hata hivyo lilipingwa na wakili wa upande wa serikali, Stella
Majaliwa.
Tukio la uporaji na mauaji hayo lilitokea Julai 11 mwaka 2007 katika
Benki ya NMB tawi la Mwanga, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment