WANANCHI WENGI WAAMINI KUWA GESI IMELETA NEEMA NCHINI TANZANIA, LAKINI WENGI WANA WASIWASI KUWA SERIKALI NA MATAJIRI WATAFAIDIKA ZAIDI.
3 Juni 2014, Dar es Salaam: Wananchi wanne kati ya watano wanaamini kuwa
mafuta na gesi yatawanufaisha wao, watoto wao na nchi yao kwa ujumla.
Wakati huo huo, wananchi wanne kati ya kumi (37%) wanaamini kuwa
viongozi wa Serikali na matajiri ndio wataofaidika zaidi. Pia, zaidi ya
nusu (55%) wangependa baadhi ya mapato ya mafuta na gesi wapewe
wananchi moja kwa moja kama fedha taslimu.
Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti wenye
jina la Kusimamia Maliasili: Wananchi wanasemaje? Utafiti huu ulifanywa
kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na umetokana na takwimu za Sauti za
Wananchi, utafiti wa kwanza Afrika kwa njia ya simu ya mkononi wenye
uwakilishi wa kitaifa.
Utafiti unaonesha kwamba matakwa ya wananchi ni kuwa, angalau kiasi cha
mapato ya mafuta na gesi kipelekwe moja kwa moja kwa wananchi. Mwananchi
mmoja kati ya watano (20%) angependelea kiasi kikubwa cha fedha
kipelekwa moja kwa moja kwa wananchi; wakati wananchi asilimia 18
wangependelea kuwe na mgawo sawa wa mapato kati ya serikali na wananchi.
Asilimia 17 wangependelea Serikali ipate asilimia kubwa zaidi ya mapato
kwa ajili ya kuendeleza miundombinu na huduma za kijamii na wananchi
wapewe kiasi kinachobaki.
Hata hivyo, Watanzania walio wengi (43%) wangependa mapato yote yaende
Serikalini kwa ajili ya kugharamia huduma muhimu. Isitoshe, wananchi
walipoulizwa namna wanavyoamini mapato ya rasilimali yanaweza kuleta
manufaa kwa Watanzania, nusu yao (46%) walisema mapato yatumike katika
kutoa huduma za afya na elimu, na wananchi wanne kati ya kumi (20%)
walipendekeza yatumike kwenye miundombinu au kwenye mipango ya kupambana
na umaskini (17%).
Linapokuja suala la usimamizi wa maliasili, jambo la msingi ni
kuhakikisha kuwa Tanzania haiangukii kwenye uhanga wa laana ya utajiri
wa maliasili. Uzoefu kutoka nchi nyingine unaonyesha kuwepo kwa uwazi
kuhusu mapato na mchakato kama kitu muhimu sana katika kuepuka laana
hii, pamoja na ushiriki wa wananchi katika kufanya maamuzi yanayohusu
namna mapato yanavyosimamiwa.
Hivi sasa, ingawa Watanzania wengi (64%) wanafahamu ugunduzi wa mafuta
na gesi, Utafiti wa Sauti za Wananchi ulibaini kuwa Watanzania wawili
kati ya watatu (65%) wangependa kupata taarifa zaidi. Pindi taarifa
zinapokosekana, tetesi na uvumi mara nyingi huziba pengo hilo. Ingawa
makadirio ya sasa yanasema kuwa uchimbaji mkubwa wa mafuta na gesi
hautaleta faida katika kipindi cha miaka saba hadi kumi ijayo, mwananchi
mmoja kati ya watatu (36%) anaamini kuwa makampuni ya mafuta na gesi
tayari yameshaanza kupata fedha kutokana na ugunduzi huu. Isitoshe
wananchi watatu kati ya kumi (28%) hawana uhakika kama tayari kuna
mapato kutoka kwenye mafuta na gesi au la. Aina hii ya mapengo kati ya
mitazamo na uhalisia, kama haitaangaliwa vizuri, inaweza kusababisha
wananchi kutoridhishwa na usimamizi wa maliasili.
Mjadala mwingine mkali umekuwa juu ya nafasi ya makampuni ya ndani na ya
nje ya nchi katika kuchimba mafuta na gesi. Wafabiashara wengi wamedai
kwa msisitizo upendeleo utolewe kwa makampuni ya Tanzania. Nusu ya
Watanzania (52%) wangependa kunufaika na utaalamu wa makampuni ya kigeni
katika sekta hii, lakini kwa kushirikiana na makampuni ya ndani ambayo
yanapaswa kumiliki hisa kubwa zaidi katika ushirikiano wa kibiashara
hio. Mwananchi mmoja kati ya watatu (35%) anaamini kuwa makampuni ya
ndani yapewe kipaumbele kwenye zabuni za makubaliano. Aidha, Watanzania
sita kati ya kumi (61%) wako tayari kuona mafuta na gesi yakiuzwa
kimataifa kwenye nchi zote. Hata hivyo, wananchi watatu kati ya kumi
(28%) wanafikiri gesi inapaswa kutumika nchini tu, na mwananchi mmoja tu
kati ya ishirini (5%) anafikiri mauzo ya gesi yafanyike nchi za Afrika
Mashariki pekee.
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza, alisema "Kama tunataka watu wa Tanzania
wanufaike na ugunduzi wa gesi, tunahitaji uongozi wa serikali ulio
imara, wenye uwazi na ubunifu. Kuwepo kwa mfuko huru wa utajiri wa taifa
ni sehemu moja muhimu ya ufumbuzi. Hata hivyo, tunahitaji kufikiria juu
ya njia mbadala, kama vile kupeleka fedha moja kwa moja kwa watu. Jambo
la msingi zaidi ni kuweka wazi taarifa, kusikiliza maoni ya wananchi na
kuwasiliana ili kujenga imani ya wananchi kufahamu namna fedha za gesi
inavyotumika."

No comments:
Post a Comment