UKATILI: TAJIRI ADAIWA KUMCHOMA KWA PASI MTUMISHI WAKE KWA MIAKA MITATU
Dar es Salaam. Mfanyakazi
wa ndani, Yusta Lucas (20) amekumbana na masahibu yanayofanana na yale
ya mtoto Nasra Mvungi (4) aliyekuwa amefungiwa kwenye boksi kwa miaka
karibu minne huko Morogoro. Huyu amelazwa katika Hospitali ya
Mwananyamala, Dar es Salaam akiuguza majeraha yanayotokana na kuteswa na
kufungiwa ndani kwa miaka mitatu.
Binti huyo, mwenyeji wa Mkoa wa Tabora, katika Kijiji cha Kampala amedai
kuwa amekuwa akiteswa na kufungiwa ndani ya nyumba na tajiri yake,
Amina Maige wa Mwananyamala, Kwa Manjunju katika kipindi chote hicho.
Amina anashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay kwa tuhuma hizo
na amefunguliwa jalada namba OB/RB/9967/2014.
Akisimulia masahibu yaliyompata akiwa katika Wodi Namba Tatu ya
hospitali hiyo, Yusta alisema: “Nililetwa Dar es Salaam mwaka 2010
kufanya kazi za nyumbani baada ya bosi wangu (Amina) ambaye ni binamu
yangu kuzungumza na mama yangu na kuniomba nije kumsaidia kazi
ndogondogo.”
Alisema aliishi vizuri na mwajiri wake huyo, lakini mwaka 2012 ndipo
mambo yalipoanza kubadilika akidai kuwa Amina alianza kumwadhibu kwa
kumng’ata na kumchoma kwa pasi kila alipomtuhumu kutokufanya kazi zake
vizuri.
“Alikuwa akinichapa na kuning’ata sehemu mbalimbali wakati mwingine
usoni, pia kunichoma kwa pasi yenye moto kila aliponituhumu kutokufagia
au kupiga deki vizuri.”
Hakuwahi kupelekwa hospitali
Alisema licha ya kupata vidonda kutokana na adhabu hizo, mwajiri wake
huyo hakuwahi kumpeleka hospitali na pale alipoona hali ni mbaya
alimnunulia dawa... “Tunaishi wawili tu baada ya kuondoka mumewe na
mtoto wake kumpeleka shule ya bweni... niliugulia hadi nikapona bila mtu
mwingine kufahamu.”
“Akienda kazini anafunga geti na kunikataza kufungua hata kama mtu
atagonga… sokoni nilikuwa naenda siku ambazo yeye yupo tu na huwa
akiniamrisha niende haraka na kurudi pasipo kuzungumza na mtu yeyote.”
Alisema mwajiri wake huyo alikuwa akituma pesa za mshahara wake kwa mama
yake akisema ndiye anayepaswa kulipwa, jambo ambalo anadhani limemfanya
mama yake kuhisi mwanaye yuko katika mikono salama... “Kila alipotuma
alipiga simu na kunipa niongee na mama kuhakikisha kama zimefika huku
akinisimamia na baada ya hapo anachukua simu.”
Ataka kurudi kwao
Binti huyo ambaye sehemu kubwa ya mwili wake ina alama za kung’atwa meno
na majeraha ya kuchomwa na pasi, alisema: “Ninaomba mtu yeyote mwenye
hela, nataka nikitoka hapa hospitali nirudi Tabora kwa mama. Nina shaka
na maisha yangu hapa kwa huyu mama… sitaki tena kubaki Dar es Salaam
kutokana na mateso ninayoyapata.
Polisi wasema
Mkaguzi Msaidizi wa Dawati la Jinsia Polisi Mkoa wa Kinondoni, Prisca
Komba alisema taarifa za binti huyo ziliwafikia baada ya majirani
kupeleka taarifa hizo katika Kikundi cha Kipange kilichopo Kwa Manjunju
ambacho nacho kilitoa taarifa polisi na ndipo mtego wa kumnasa mwanamke
huyo ukawekwa.
Majirani walichukua hatua hiyo kutokana na kusikia kelele za kilio mara
kwa mara zikitokea ndani ya nyumba ya mtuhumiwa. “Tumekagua makovu na
majeraha mbalimbali yaliyo katika mwili wake na kupata jumla kuwa yako
91,” alisema Komba na kuongeza:
“Toka jana amekuwa akinitaka nisiondoke mbali naye amekuwa na hofu,
lakini sasa afadhali kidogo baada ya kumpatia ushauri na kumhakikishia
kwamba hapa yuko salama.”
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Thobias Edoyeka alisema suala
hilo linashughulikiwa na polisi pamoja na ustawi wa jamii, kauli
iliyoungwa mkono na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mwananyamala, Rose Temu
ambaye alisema wanafuatilia kwa karibu matibabu yake pamoja na usalama
wake. “Hali yake ikishaimarika na kujiridhisha kuwa anaendelea vizuri,
tutakuwa na jukumu la kumuunganisha na familia yake,” alisema.
Ofisa Muuguzi Msaidizi Wodi Namba Tatu ambayo ni ya kinamama, Rose Mussa alisema Yusta anaendelea vizuri.
“Anaendelea vizuri kwa kweli, jana (juzi) hakuwa hivi alikuwa mwoga
hawezi kujieleza tofauti na leo (jana)… bado anaendelea na vipimo,
tutakapoona anafaa kuruhusiwa tutafanya hivyo na kumkabidhi kwa ustawi
wa jamii.”
No comments:
Post a Comment