Viongozi
wakuu wa CUF wakionyesha mshikamano baada ya kuchaguliwa kukiongoza
chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Wa pili kulia ni
msimamizi wa uchaguzi huo Awadh Ali Said (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Mkutano Mkuu
wa CUF Taifa umemchagua tena Katibu Mkuu wa Chama hicho kuendelea na
wadhifa huo kwa kupata kura 675, sawa na asilimia 99.5 ya kura
zilizopigwa.
Mkutano huo
pia umemchagua Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa kwa
kupata kura 659 sawa na asilimia 95.5 na kumshinda mpinzani wake Chifu Lutalosa Yemba aliyepata kura 30 sawa na asilimia 4 nukta 3.
Aidha
mkutano huo umemchagua Mhe. Juma Duni Haji kuwa Makamu Mwenyekiti wa
Chama hicho kwa kupata kura 662 sawa na asilimia 99.25.
Akizungumza
baada ya kutangazwa mshindi Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif
Sharif Hamad, amewapongeza wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumpa tena ridhaa
ya kuongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Wakati wa Kampeni.
Mapema
akizungumza katika kampeni za kuomba kuchaguliwa tena kuwa Katibu Mkuu
wa Chama hicho, Maalim Seif amesema siri ya mafanikio yake kisiasa ni
kutokana na kujiamini kwake kuwa kiongozi, kuwa mkweli na kuwa na
dhamira njema kwa wananchi.
Akijibu hoja
za wajumbe wa mkutano huo Maalim Seif amewataka viongozi wa chama hicho
kutotangaza kuhudhuria kwa viongozi wa kitaifa kwenye mikutano ya
hadhara hadi pale wenyewe watakapothibitisha kuhudhuria, ili kuepusha
wananchi kutoamini utendaji wa viongozi hao.
Mgombea wa
nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Juma Duni Haji amesema
iwapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo atashirikiana na viongozi wengine
wa kitaifa pamoja na wananchi kuhakikisha kuwa chama kinapata maendeleo
zaidi.
Chifu Yemba amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kutetea demokrasia ya kweli ndani ya chama na taifa kwa ujumla.
Chifu Yemba ambaye ni mwanasayansi kitaaluma, pia ni Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Shinyanga Mjini.
Prof. Lipumba amesema akichaguliwa atahakikisha anatembelea nchi nzima kuimarisha chama kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Aidha
amesema atafanya juhudi za ziada kuona kuwa Tanzania inakuwa na Muungano
wa kuheshimiana baina ya pande mbili za Muungano (Tanzania Bara na
Zanzibar).
Amesema
wanawake watapewa nafasi ndani ya kamati tendaji ya chama kuondosha
dhana ya mfumo dume unaodaiwa kuwepo katika ngazi za juu za uongozi.
Mgombea
mwengine wa nasafi ya Mwenyekiti wa CUF Taifa M’bezi Adam Bakar,
amejitoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kubakia wagombea wawili wa
nafasi ya Mwenyekiti.
Mwakilishi
wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu aliteuliwa kuwa
mwenyekiti wa muda wa kuongoza uchaguzi huo uliosimamiwa na mwanasheria
Awadh Ali Said.
No comments:
Post a Comment