INASIKITISHA: MGONJWA WA SARATANI ALIYETELEKEZWA AFARIKI DUNIA
Dar es Salaam. Mgonjwa wa saratani ambaye alidai kupewa tiba feki za mionzi katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (OCRI), Pendo Shoo amefariki dunia juzi wilayani Karatu akiwa safarini kuelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro kwa wazazi wake.
Mdogo wa Pendo, Digna Shoo, alisema dada yake alifariki juzi, saa nne usiku wakati wanafamilia wakimfanya maombi.
“Alianza kubadilika ghafla wakati tukiwa katikati
ya maombi, alilegea na mgongo wake ukawa kama unapinda hivi, tukamshika
na tukamweka kitandani,” alisema.
Digna alisema kwamba baada ya kumweka kitandani
mtumishi wa Mungu aliyekuwa nyumbani hapo alimwombea na hazikupita
dakika nyingi akakata roho. Alisema Pendo alikwenda Karatu akitokea Dar
es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita, kipindi ambacho hali yake ilikuwa
imeshatetereka sana kiasi cha kushindwa kutembea mpaka apate msaada wa
mtu karibu.
“Wakati tunatoka Dar es Salaam kuja Karatu, hali
yake ilikuwa imeshakuwa mbaya, alikuwa hawezi kutembea bila kumpa
‘support’ (msaada) alikuwa anapepesuka,” alisema Digna.
Digna alisema safari ya dada yake haikuwa imelenga
kuishia Karatu, bali walikuwa wanaelekea Kirua Vunjo, Kilimanjaro
ambako ni nyumbani kwao alipozaliwa, lakini mauti yalimkuta msichana
huyo kabla hajafika.
Kwa maelezo ya Digna, Pendo alikuwa amekata tamaa
ya kuishi kutokana na saratani hiyo kusambaa katika matiti yake mawili
na kumsababishia vidonda vilivyompa maumivu makali.
Itakumbukwa kwamba gazeti hili liliwahi kuripoti
mara mbili taarifa kuhusu Pendo; kwanza ni ile iliyohusu mgonjwa huyo
kupewa dawa feki ambazo badala ya kumtibu zilimsababishia madhara zaidi
na pili ni kuhusu kunyanyapaliwa baada ya taarifa ya awali kuandikwa
gazetini.
Pendo alianza kupata tiba OCRI Novemba mwaka jana
baada ya kupata rufaa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini katika
mchakato wa tiba yake, alitozwa kiasi cha Sh1.34 milioni na mtumishi wa
OCRI, Almasi Matola kinyume na taratibu.
Baada ya gazeti hili kuchapisha habari hiyo, Mei
20 mwaka huu alikwenda katika hospitali hiyo kupata tiba zaidi, lakini
alinyanyapaliwa na wahudumu wa OCRI na akielezwa kwamba vipimo
alivyochukuliwa awali vilikuwa havionekani.
“Niliamua kurudi hospitali nikapime tena na
nilitoa damu kwa ajili ya vipimo, lakini nilipokwenda tena kuchukua
majibu walidai damu yangu imepotea. Kwa hiyo nililazimika kuanza upya,
nilitoa damu tena na vipimo vyote vikawa tayari kama X-ray, Ultra sound
na nikavipeleka kwa daktari,” alisema Pendo kabla ya kukutwa na mauti.
Alisema alipatwa na hofu zaidi baada ya kwenda kwa
daktari wake Dk Dominista Kombe, ambaye alipaswa kumpa matokeo ya
vipimo, lakini alishangaa daktari huyo alipomjibu kwamba, “Majibu yako
utayajua hukohuko,” akimaanisha kwenye chumba cha tiba ya mionzi.
Alisema alipofika chumba cha tiba ya mionzi muuguzi aliyekuwapo
alimwambia asubiri kwenye foleni hadi atakapoitwa jina, lakini alikaa
zaidi ya saa nzima bila faili lake kuitwa. Alisema baadaye muuguzi
alirudi na kumwambia aende nyumbani kwa sababu wagonjwa ni wengi. Lakini
wagonjwa wengine waliokuwa kwenye foleni hawakupewa maelekezo hayo na
waliendelea kusubiri.
Kutokana na hali hiyo, Pendo aliapa kwamba
asingeweza kwenda tena OCRI na badala yake kuamua kusaka tiba asili na
kwenda makanisani kwa ajili ya maombi na maombezi. Mara ya mwisho,
marehemu aliwasiliana na gazeti hili akiwa safarini kwenda Karatu ambako
amefikwa na mauti.
Uongozi wa OCRI
Mkurugenzi wa OCRI , Dk Twalib Ngoma alisema suala
la Pendo lilishafanyiwa kazi na ripoti ya tukio lote ipo kwenye bodi
na matokeo ya ripoti hiyo huenda yakatolewa hivi karibuni.
“Mimi nipo likizo...lakini suala hilo
lilishafanyiwa kazi kwa sababu hatuwezi kuacha hivihivi lipite bila
kuchukua hatua. Tunalifanyia kazi kwa undani kitaasisi,” alisema Dk
Ngoma jana kupitia simu yake ya mkononi.
Aliongeza: “Tunajua kuwa gazeti la Mwananchi lilikuwa na nia njema, lakini siwezi kuhukumu na lazima taasisi ifanye uchunguzi.”
Mkurugenzi wa Tiba wa OCRI, Dk Diwani Msemo
alisema uongozi ulichukua hatua za kumpigia simu Pendo na kumwambia
arudi hospitali ili akabadilishiwe daktari na dawa, lakini Pendo
aliwaambia kwamba yuko Karatu.
“Tulimpigia simu Pendo ili aje atoe na maelezo yake, tusingeweza kuhukumu kwa maelezo ya upande mmoja tu,” alisema Dk Msemo.
Alisema nia ya OCRI ilikuwa ni kusimamia matibabu
ya Pendo ikiwemo kumpa tiba akiwa nyumbani kwa sababu taasisi hiyo ina
kitengo cha kutoa tiba ya aina hiyo.
Alisema sambamba na hilo, uongozi ulichukua
maelezo ya madaktari waliomhudumia Pendo na muuguzi anayedaiwa kupokea
fedha na kutoa dawa feki.
Alisema maelezo ya Matola aliyoandika kwa uongozi
wa OCRI, ni kuwa dawa aliyompa Pendo ilibakizwa na mgonjwa mwingine
ambaye alitaka kurejeshewa fedha zake ndiyo maana alichukua fedha hizo
kwa mgonjwa.
Hata hivyo, Dk Msemo alisema OCRI haina mamlaka ya kuchukua
fedha kwa mgonjwa ili kumpa tiba na badala yake, dawa zilizobaki
hutakiwa kurudishwa kwenye kitengo cha dawa.
“Tumewapa barua za maonyo, wengine tumewabadilisha
vitengo na hatua zaidi zilikuwa zinaendelea kuchukuliwa lakini mauti
yamemkuta kabla,” alisema.
No comments:
Post a Comment