
CHUO CHA UALIMU KOROGWE
Serikali imepandisha maradufu ada kwa wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vya ualimu nchini kuanzia muhula ujao wa masomo.
Ada hizo kwa wale wa ngazi za cheti na
stashahada ambazo zimeongezwa kwa karibu mara mbili au zaidi ya zile
zilizokuwa zikilipwa awali. Uamuzi huo ambao huenda ukawaathiri zaidi
wanafunzi ambao waliona ualimu kama kimbilio, unaelezwa na baadhi ya
wadau wakiwamo walimu, wanafunzi na hata wakufunzi wa baadhi ya vyuo
nchini kuwa ni wa ghafla.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakufunzi,
uamuzi huo umetolewa kupitia waraka wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi na unatarajiwa kuanza kutekelezwa muhula wa pili wa masomo
utakaoanza Julai 2, mwaka huu.
Kabla ya kupandishwa kwa ada hizo,
wanafunzi wanaosomea ualimu kwa ngazi ya cheti walikuwa wakilipa
Sh200,000, lakini sasa watalazimika kulipa Sh300,000, ikiwa ni ongezeko
la asilimia 50.
Kwa wale wanaochukua stashahada
watalazimika kulipa Sh400,000 kwa masomo ya Sanaa na Sh600,000 kwa
masomo ya Sayansi kutoka Sh200, 000 za awali.
Mhasibu wa Chuo cha Ualimu cha Mtwara,
aliyekataa kutaja jina lake kwa kuwa siyo msemaji wa chuo hicho,
alithibitisha kupokea waraka wa Serikali unaowataka kupandisha ada,
lakini alisisitiza kuwa Mkuu wa Chuo ndiye angeweza kufafanua zaidi
kuhusu ongezeko hilo.
“Taarifa hizo ni za kweli ada imepanda,
kama umezipata kutoka wizarani hivyo ndivyo ilivyo kwa hiyo huna sababu
ya kupata taarifa zaidi kutoka kwetu,” alisema mhasibu huyo.
Awali, habari zilizolifikia gazeti hili
zilieleza kuwa Serikali imefikia uamuzi huo kutokana na uhaba wa fedha
na ugumu wa kuviendesha vyuo hivyo.
Habari zinasema kwa muda mrefu sasa,
Serikali imekuwa ikidaiwa na wazabuni fedha nyingi, jambo ambalo
limeathiri pia uendeshaji wa vyuo vikiwamo vya ualimu.
Baadhi ya wakufunzi wameeleza kuwa fedha
za ada sehemu yake itatumika kutatua matatizo ya uhaba wa fedha ambao
umekuwa ukiwakabili na hivyo kuathiri utoaji wa huduma zikiwamo za
vyakula.
Wizara ya Elimu
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema viwango vilivyoongezwa siyo vikubwa
ikilinganishwa na hali ya ugumu wa maisha ilivyo sasa nchini.

Baadhi ya wahitimu wa chuo cha Ualimu.
“Unamweka mtu mwaka mzima anakula,
analala, anasoma…kweli unaona hiyo ada hiyo ni kubwa? Bado siyo kubwa
kiasi cha kushtua watu,” alisema Bunyazu.
Aidha, Bunyazu alisema kuwa wanafunzi
watakaopata daraja la kwanza katika masomo ya Sayansi na Hisabati na
kuingia katika vyuo vya ualimu vya Serikali watasomeshwa bure na wale
watakaopata daraja la pili na la tatu watapewa mkopo.
Wengine wazungumza
Meneja wa Utafiti na Uchambuzi wa Sera
wa Shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventura akizungumzia suala hilo
jana, alisema kuwa siyo kweli kwamba serikali haina fedha za kutosha
ndiyo maana inaongeza ada, ila inadhani kuwa idadi ya walimu waliopo
inatosha.
“Serikali imeamua kupandisha ada kwa
kudhani kuwa walimu waliopo wanatosha, lakini ikumbuke kuwa kuna walimu
wengi wazee wanaostaafu kila mwaka, wengine hawaripoti shuleni, hivyo
tunahitaji kuwa na benki ya walimu,” alisema Boniventura.
No comments:
Post a Comment